Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Magufuli: msitishike na kauli ya ‘maagizo kutoja juu’
Habari za SiasaTangulizi

Rais Magufuli: msitishike na kauli ya ‘maagizo kutoja juu’

Spread the love

RAIS John Magufuli amewataka wafanyabiashara kutokubali kutishwa na msemo wa ‘maagizo kutoka juu’. Anaandika Regina Mkonde … (endelea).

Amewataka wafanyabiashara hao kutotekeleza wanachoamriwa, hadi pale wahusika watakapotaja aliyewaagiza.

Rais Magufuli ametoa wito huo wakati akizungumza na wafanyabiashara zaidi ya 1,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini, leo tarehe 7 Juni 2019 Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Amewaeleza wafanyabiashara hao kuwa, serikali yake ina wathamini na kwamba, wasiwasikilize baadhi ya  watumishi yeyote wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wanaotumia msemo wa maagizo kutoka juu kudai pesa.

Amesema, kama wahusika hao hawatataja aliyewaagiza, wafanyabiashara hao wasitoe hata senti tano, kwani inawezekana wameagizwa na pepo linalokaa juu.

“Niwaombe kwa dhati serikali hii ina wathamini sana, na kamwe asije mtu wa TRA akasema ni maagizo ya juu.

“Mwambie nitajie huyo wa juu aliyekuagiza, usipotaja sikupi hata senti tano sababu inawezekana labda ni maagizo ya pepo ambalo linakaa juu.

“… limemuagiza ukiwa umelala, limemuingia kichwani. Yeye analiona liko juu na kweli liko juu halioni, na wewe unakubali tu .Nyie mko Tanzania na ni free country, mwambie tunataka hayo maagizo.”

Rais Magufuli amesema, wakati mwingine baadhi ya wafanyabiashara wanatengeneza mazingira ya kunyanyaswa, kwa kuendekeza kutoa rushwa ili kukwepa kulipa kodi.

Amewatala wafanyabiashara hao kukataa kulipa kodi ambayo ni kubwa ukilinganisha na mitaji pamoja na mapato ya biashara zao.

“Lakini ni kweli wapo wengine wafanyakazi wa TRA, niwaombe wafanyabiashara msitoe rushwa kataeni rushwa, kunyanyswa kwenu mnakujenga wenyewe. Anapokuomba rushwa kataa, anapokupa makadirio ya juu ukilinganisha na mtaji wako kataa , ‘apeal’ hata kwa kamishna mkuu,” ameagiza Rais Magufuli.

Agizo hilo la Rais Magufuli limekuja baada ya baadhi ya wafanyabiashara kuilalamikia TRA pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwamba baadhi ya watumishi wake wamekuwa wakitumia msemo wa ‘maagizo kutoka juu’ kuwadai kodi na au kubeba fedha zao kwa lazima.

Kufuatia Malalamiko hayo, Rais Magufuli amemtaka Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere kusimamia wafanyakazi wake vyema ili kuhakikisha kwamba hawanyanyasi wafanyabiashara kwa kigezo cha kudai kodi.

“Haiwezekani unaenda kudai kodi, unaenda na bunduki, Kamishna akasimamie watu wake, sipendi kuona mfanyakazi wa TRA ananyanyasa mfanyabiashara, na sitaki mfanyabiashara anyanyase mfanyakzi wa TRA, tufanye kazi kwa pamoja, wale wana wajibu wa kukusanya fedha ili watanzania waishi vizuri,” ameagiza Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amewataka wafanyabiashara wenye madeni na malimbikizo ya kodi, na wale waliokwepa kulipa kodi, kuwa waungwana kwa kujisalimisha kwa TRA ili walipe wazungumze namna ya kulipa madeni yao.

“Saa nyingine haya madeni ni ya nyuma ukae mzungumze. Kwa hiyo nisamehe hapa hapa, muwasikilizeni , biashara ni mahusiano si uadui,” amesema Rais Magufuli.

Akizungumzia kuhusu mkutano huo, Rais Magufuli amesema umemfumbua macho kwa kuwa baadhi ya walioshiriki wamekuwa huru kueleza changamoto wanazokabiliana nazo katika mazingira ya ufanyaji biashara.

Rais Magufuli amemtaka Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Salum Shamte kuhakikisha kwamba anapanua wigo wa utendaji wa taasisi hiyo, ili iweze kufikia wafanyabiashara wengi nchini, kwa kuwa ndio chombo pekee cha uwakilishi wao.

“Kwa leo mimi nimejifunza sana sana na mkutano huu umekuwa mzuri sana, na ndio maana ninarudia wito wangu kwa Bwana shamte, nafikiri sasa hivi imefikia wakati tuwe na chombo chenye uwakilishi mkubwa, kuna baadhi ya masuala hayafikiwi na serikali, zinaishia huko,” amesema Rais Magufuli na kuongeza.

“Mimi najua ningekaa kwenye kikao chenu msingeniambia masuala ya rushwa, nisingepata maneno kwamba watu wanafungiwa mabasi kwa sababu ya mtu mmoja wa TRA ameamua.Ombi langu mkalifanye liwe kubwa ili kusudi mkazungumze yale ya ukweli yanayogusa Watanzania.”

Wakati huo huo,Rais Magufuli amewataka wafanyabiashara  kuwafichua wanaowakwamisha katika biashara zao kwa kigezo cha kutaka rushwa.

Pia, amesema yuko tayari kutoa mchango wake wa hali na mali kwa wafanyabiashara wanaotaka kusafirisha bidhaa zao nje ya nje.

Ameeleza kuwa, kama wafanyabiashara watahitaji ndege ya kusafirishia mizigo, serikali yake iko tayari kununua.

“Wale wanaokaamisha kusafirisha ndio muwaseme, hata kwenye tv nenda kazungumze mtatusaidia, kama mnataka mtushauri tununue ndege ya cargo si tutanunua. Nataka hizi biashara mzishike ninyi, dhamira yangu nitafurahi sana kama sisi tukiondoka tuwe na watu zaidi ya 100 ambao ni bilionea na hii inawezekana kama tukiamua,” amesema Rais Magufuli.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!