DAKTARI John Magufuli, Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), amesema hakuna haja ya watu kuzaa kwa mpango kwa kuwa Serikali yake inatoa elimu bure. Anaripoti Mwandishi Wetu, Singida … (endelea).
Mgombea huyo wa CCM katika nafasi ya Urais wa Tanzania kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano wa tarehe 28 Oktoba 2020 ametoa kauli hiyo leo tarehe 1 Septemba 2020, katika mkutano wake wa kampeni ulioanyika Ikungi mkoani Singida.
“Tunataka watoto wasome bure, ndio maana siku zote nilikuwa nasema zaeni hakuna kuzaa kwa mpango, matiti ya kunyonyesha watoto tunayo, maziwa tunayo na wanaume wapo wakina mama wapo na shule wanasoma bure serikali ipo,” amesema Rais Magufuli.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amewataka wakazi wa Ikungi na Watanzania kwa ujumla bila kujali tofauti za vyama vya siasa, kumpigia kura ili Serikali yake iendelee kutoa elimu bure.
“Asije akaja mwingine akageuza badala ya katoa elimu bure, watoto wakaanza kudaiwa, tutakuwa tunarudi nyuma.”
“Kwa nini turudi nyuma tulikotoka? Na ndio maana tunasema katika miaka mitano ijayo, tutatoa elimu bure ndio maana tunaomba ndugu zangu mturudishe,” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli anaendelea na kampeni zake alizozizindua Jumamosi tarehe 29 Agosti 2020 jijini Dodoma, ambapo leo asubuhi alianzia Bahi mkoani Dodoma na kisha kuendelea Ikungi mkoani Singida.
Leave a comment