July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli ahamia rasmi Dodoma

Rais John Magufuli akijiandikisha kwenye daftari ya kupiga kura katika makazi yake mpya Chamwino, Jijini Dodoma

Spread the love

RAIS John Magufuli ametangaza kuhamia rasmi kwenye Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa na Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, leo tarehe 12 Oktoba 2019.

Taarifa ya Msigwa imesema Rais Magufuli ametangaza uamuzi huo, alipokwenda kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kwenye Kituo cha Sokoine wilayani Chamwino, Dodoma. 

Rais Magufuli ameeleza kuwa, kuanzia sasa shughuli zake atazifanyia jijini humo.

“Mimi nilikuwa Katavi, nimeamua kuja kujiandikisha nyumbani sababu hapa ndio nyumbani kwangu, na nimeshakuja rasmi hapa. Kwa hiyo kila siku tutakuwa tunaonana hapa. Ndio maana nimeona nije nijiandikishe mimi pamoja na mke wangu,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amehamia jijini Dodoma akitokea Ikulu ya Dar es Salaam, waliyokokaa watangulizi wake, Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere hadi Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete.

Ikulu hiyo ilijengwa na Wajerumani mwaka 1891 kabla ya Tanzania Bara (Tanganyika) kupata uhuru, tarehe 9 Desemba 1961, na kuungana na Zanzibar mwaka 1964 na kuwa nchi ya Tanzania.

Rais Magufuli amehamia Dodoma ili kumuenzi Mwalimu Nyerere, aliyeanzisha wazo la Makao Makuu ya Nchi kuwa jijini humo.

Kuhusu zoezi la uandikishaji orodha ya wapiga kura, Rais Magufuli amewahimiza Watanzania kujiandikisha, ili waweze kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa watakao ona wanafaa.

error: Content is protected !!