September 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askofu Kakobe aombea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Askofu Zacharia Kakobe

Spread the love

ZACHARY Kakobe, Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) ameongoza sala ya kuombea uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa mwakani. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Sala hiyo imefanyika leo tarehe 12 Oktoba 2019, katika Kongamano la Kwanza la Jukwaa la Kumhubiri Kristo (JKK) lililofanyika kwenye Kanisa la Ushauri wa Biblia na Vituo vya Maombezi (BCIC) jijini Dar es Salaam.

Akiongoza sala hiyo, Askofu Kakobe amemuomba Mungu kutoa baraka zake ili chaguzi hizo zifanyike kwa amani.

“Na kwa jina la Yesu Kristo mkono wake hodari ukapate kufungua mambo yote. Uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwakani, vyote vifunikwe na maongozi yako na yasiwe maongozi ya wanadamu,” ameomba Askofu Kakobe.

Wakati huo huo, Askofu Kakobe amemkabidhi Rais John Magufuli kwa Mungu, na kumuomba amjalie hekima ili aliongoze vema taifa.

“Kama unavyotuamuru tuombe kwa ajili ya wote wenye mamlaka, kwa sasa tunamkabidhi Rais Magufuli mkono wako uwekwe juu ya kichwa chake. Wewe ukiweka mkono wako, umesema si mfupi hata ushindwe kuokoa.

 Kila kinachopungua ndani yake ukijaze sasa, jaza hekima yote ya maongozi, jaza kila kinachohitajika katika uongozi, mpe kuisikia sauti yako apate kujua anatuongoza kwenda wapi na kwa namna gani,” ameomba Askofu Kakobe.

Askofu Kakobe amemuomba Mungu amzidishie unyenyekevu Rais Magufuli, pamoja na kumpa maono yatakayoipeleka Tanzania kwenye mafanikio.

“Tumemsikia rais wetu akisema naomba mniombee, sio rahisi katika dunia kupata mtu wa ngazi yake anayeweza kukutumaini wewe na kutaka kukuombea. Wakati yeye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Nchi anaweza kutoa maagizo tu yakafanyika, lakini amejua wazi pasipo wewe, yeye hawezi kufanya jambo lolote. Unyenyekevu huo uzidishe kwake na wote wenye mamlaka,” ameomba Askofu Kakobe.

error: Content is protected !!