Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Prof. Lipumba azidi kujianika  
Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba azidi kujianika  

Prof. Ibrahim Lipumba na Maalim Seif Shariff Hamad (picha ndogo)
Spread the love

MWENYEKITI asiyetambuliwa na wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, amemtuhumu Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad, kuwa analenga kukidhoofisha chama hicho n ahata kukizika kabisa. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo tarehe 21 Februari, Lipumba anasema, Maalim Seif ndio kikwazo cha kumaliza gogoro linalokitafuta chama hicho kikuu cha upinzani, Visiwani.

Anasema, “zimekuwapo juhudi kadhaa zinazolenga kumaliza mgogoro huu. Lakini Maalim (Seif Seif Shariff Hamad), amekuwa kikwazo cha kufikia malengo hayo.”

Anasema, “…kama malengo ya Maalim ni kujenga chama, tungekutana na kutafuta suluhu. Lakini mwenzetu hataki hilo. Anataka kukivuruga chama chetu. Ndio maana kuna wakati amewahi kutamka kwamba kama Lipumba akitokea hapa, mimi nitaondoka.”

Prof. Lipumba alijiuzulu uenyekiti wa chama hicho, kwa hiari yake, katikati ya kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa 25 Oktoba 2015.

Katika barua yake ya kujiuzulu, Prof. Lipumba alimjulisha Maalim Seif – katibu wa mamlaka iliyomchangua kuwa mwenyekiti – kuwa amejizulu wazifa wake.

Lipumba hakuwa ameomba kujiuzulu. Alikuwa anajulisha uamuzi  ambao tayari alishachukua na kuutekeleza.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinasema, kabla ya kuwasilisha barua yake kwa Malim Seif, watu wa aina mbalimbali na rika tofauti, walimuomba Lipumba abadilishe uamuzi wake wa kujiuzulu. Alikataa.

Alisema, “sitarudi nyuma. Nafsi imenisuta. Nang’atuka.” Akaongeza, “najua kuwa uamuzi wangu utawaumiza wengi, lakini CUF ni taasisi. Nitatoa ushirikiano nitakapohitajika. Nitabaki kuwa mwanachama wa kawaida.” Akatoka ofisini. Akaacha kufanya shughuli za chama.

Baraza kuu lilipokutana lilijulishwa na katibu mkuu juu ya kujiuzulu kwa Lipumba. Likaunda kamati ya muda kukiongoza chama. Kamati ilikuwa chini ya uenyekiti wa Twaha Taslima, Abubakar Khamis Bakary na Severina Mwijage.

Prof. Lipumba anakiri kuwa Maalim Seif, ana nguvu kubwa sana za kisiasa nchini na kwamba hatma ya baadaye ya chama hicho, iko mikononi mwa mwanasiasa huyo.

Kuibuka kwa Prof. Lipumba kuzungumzia anachokiita “mustkabali wa baadaye wa CUF,” kumekuja siku tangu yeye na genge lake, wapigwe mweleka mahakamani na “CUF taaasisi,” inayoongozwa na Maalim Seif, kufuatia mahakama kuifuta bodi yake ya wadhamini.

Katika shauri hilo, lililofunguliwa na Mbunge wa Malindi (Unguja), Alli Salehe Alberto, mahakama kuu, kanda ya Dar es Salaam imesema, “bodi ya wadhamini ya Lipumba, imekosa uhalali kisheria na haipo kwa mujibu wa sheria.”

Salehe alifungua shauri hilo mahakamani, lililopachikwa jina la “kesi ya bodi feki,” mwaka 2017.

Katika mkutano wake huo na wanahabari, Prof. Lipumba amesema, miongoni mwa misimamo ya Maalim Seif inayohatarisha uhai wa chama hicho ni pamoja na hoja yake ya Muungano wa Mkataba.

Lipumba amedai kuwa msimamo huo unakinzana na masharti ya usajili wa vyama vya siasa na kwamba jambo hilo likiachwa kuendelea kujadiliwa ndani ya CUF, basi linaweza kusababisha chama hicho kufutiwa usajili.

Amesema, “hana lengo la kukijenga chama cha CUF; na alishasema wanafanya maamuzi magumu. Anataka kuaminisha jamii, kwamba bila yeye CUF haipo. CUF ni chama cha kudai haki na kitaendelea kuwepo.”

Lipumba anadai kuwa tofauti kubwa ya kisisasa kati yake na Maalim ni suala la Muungano wa Mkataba.

Anasema, “yeye (Maalim Seif) ni muumini wa Muungano wa Mkataba. Sasa nikamueleza, mbona unataka kutuletea matatizo? Unataka chama chetu kifutwe; kwa kuwa chama chetu kimeasisiwa na kusajiliwa kwa masharti kwamba kinakubali kuwepo kwa Muungano wa Tanzania.”

Pia Prof.  Lipumba anaeleza kukerwa na hatua ya Maalim Seif kuama kutotoa ushirikiano na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Amesema, hatua ya Maalim Seif kufanya kikao cha wajumbe wa Baraza Kuu la uongozi na kuteua wajumbe wa Bodi ya Udhamini bila kushirikisha Ofisi ya Msajili wa Vyama linahatarisha chama hicho.

Anasema, “taasisi ya umma inayoshughulikia mambo ya vyama ni msajili wa vyama vya siasa, na sisi katika mikutano yetu mikuu tunaalika msajili wa vyama vya siasa.”

Anaongeza: “Ubaya wa msajili ni baada ya kufanya usajili wote na kuisoma Katiba ya CUF na kusema, mwenyekiti halali ni Lipumba aliteuliwa mwaka 2014, sasa imekuwa msajili hajui kazi.”

Hata hivyo, kinyume na madai ya Lipumba, Msajili wa vyama hana mamlaka ya kuwapangia wenye chama nani awaongoze na hivyo pia hana mamlaka ya kumrejesha madarakani kiongozi aliojiuzulu au kukataliwa na wanachama.

Prof. Lipumba amemtaja Maalim Seif kama mfa maji ambaye hataki kufa peke yake bali anatafuta wa kuangamia naye.

Amemtuhumu kuwa anataka kuisababisha matatizo Zanzibari. Hakufafanua.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!