Saturday , 15 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mahakama kuhitimisha safari ya Prof. Lipumba kisiasa?
Habari za SiasaTangulizi

Mahakama kuhitimisha safari ya Prof. Lipumba kisiasa?

Prof. Ibrahim Lipumba
Spread the love

KESHO tarehe 22 Februari 2019, Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, anaweza kuhitimisha ama kuhuisha safari yake ya kisiasa aliyoianza zaidi ya miaka 20 iliyopita. Anaandika Jabir Idrissa…(endelea).

Ikiwa ni siku tatu baada ya kubwagwa na Kambi ya Maalim Seif Shariff Hamad, katibu mkuu wake baada ya Bodi ya Wadhamini aliyoiunda ‘kufyekwa’ na Mahamaka Kuu, kesho anajaribu bahati yake nyingine.

Mahakama Kuu, Kanda Maalum ya Dar es Salaam inatarajiwa kutoa hukumu kwamba, Prof. Lipumba ni mwenyekiti halali wa CUF ama badili. Hukumu ya kesho inaweza kumpa mwelekeo mpya wa kisiasa Prof. Lipumba.

Kwa sasa Prof. Lipumba anatambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kama Mwenyekiti wa CUF wakati ndani ya chama hicho, wapo wanaompinga kwa kuwa, alijiuzulu bila kushurutishwa.

Kwenye kesi inayotarajiwa kutolewa hukumu hiyo kesho, Prof. Lipumba ameshitakiwa kuwa si mwenyekiti halali wa CUF kwa kuwa, alijiuzulu kwa hiari yake kupitia tamko lake kwa waandishi wa habari hapo tarehe 5 Agosti 2015.

Kwenye andishi lake hilo Prof. Lipumba alisema, hawezi kushika wadhifa huo kutokana na kukosa ushirikiano wa viongozi wenzake.

Alisema namna chama kinavyokwenda, nafsi yake inamsuta kuendelea kuwa kiongozi wake; ila anakusudia kubakia mwanachama muaminifu na iwapo chama kitaridhia awe tu mshauri wake.

Prof. Lipumba alishikilia uamuzi wake wa kujiuzulu licha ya kunasihiwa na viongozi wenzake wa juu akiwemo Katibu Mkuu Maalim Seif Shariff Hamad.

Aliambiwa kwamba, wakati ule haukuwa muafaka kwake kuondoka kwani chama kilikuwa kinakabiliwa na jukumu la kukamilisha maandalizi ya kushiriki uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani kwa upande wa Tanzania Bara na rais, wawakilishi na madiwani kwa Zanzibar.

Baada ya kujiuzulu na haraka kuondoka nchini, kulisambazwa picha kwenye mitandao ya kijamii zikimuonesha anakula raha pamoja na watu walioonekana kama mawakala wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Baadaye ilifahamika alikuwa nchini Rwanda.

Hata hivyo, baada ya kukaa nje ya chama na kiti chake kwa miezi 10, alijitokeza tena na kutangaza kuwa ametengua uamuzi wa kujiuzulu na kwamba, anamsubiri katibu mkuu amweleze lini arudi kukalia kiti chake.

Hatua hiyo ilizua mzozo ndani ya CUF ambapo aliamua kukimbilia kwa Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, Jaji Francis Mutungi ambaye hatimaye alitangaza kumtambua kuwa mwenyekiti halali.

Ndipo mgogoro ulipokomaa baada ya kuungwa mkono na baadhi ya viongozi huku akipingwa na kundi kubwa la wafuasi ndani ya chama wakiongozwa na Maalim Seif.

Kwenye kesi hiyo, pia analalamikiwa msajili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika kushikilia hatamu, Prof. Lipumba amekuwa pamoja na Magdalena Sakaya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Abdul Kambaya aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mohamed Habib Mnyaa, Mussa Haji Kombo na Khalifa Suleiman Khalifa waliowahi kuwa wabunge.

Kama ilivyo kwake Prof. Lipumba, hao wengine nao walivuliwa uanachama kwa makosa ya kukihujumu chama. walikata rufaa ambazo mpaka sasa hazijasikilizwa.

Kuvuliwa uanachama kwao kulisukumwa na hatua ya Prof. Lipumba kuongoza kundi la wanachama na kuvuruga mkutano mkuu ulioitishwa tarehe 20 Agosti 2016 katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam kwa lengo la kumchagua mwenyekiti mpya na makamu wake.

Mkutano huo uliahirishwa mara tu ilipokamilisha hatua ya kupiga kura ya kuthibitisha kwamba, Lipumba ameacha mwenyewe uenyekiti.

Wiki mbili baadaye, aliongoza kundi la wafuasi wake na kuvamia jengo la Ofisi Kuu ya chama la Buguruni, Dar es Salaam na kuweka makazi yake huko.

Jumatatu wiki hii, Mahakama Kuu ilitoa uamuzi kuwa Bodi ya Wadhamini aliyokuwa ikitumiwa na Prof. Lipumba kufanya shughuli za chama ni haramu kwa kuwa, usajili wake hakukufuata sheria.

Bodi ya Lipumba iliyoongozwa na Thomas Malima ilisajiliwa tarehe 12 Juni 2017 wakati CUF Kambi ya Maalim Seif ikiwa inasubiri majibu ya ombi la kusajili bodi mpya.

Bodi halali sasa ni ile iliyokuwepo kabla ya mgogoro kuibuka ambayo wajumbe wake wengi wanamtii Maalim Seif pamoja na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Tanesco yawasha mtambo namba 8 Bwawa Julius Nyerere

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Samia: Wakuu wa mikoa, wilaya wanaendeleza ubabe

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema bado wakuu wa wilaya na...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Ramaphosa achaguliwa tena kuwa rais Afrika Kusini

Spread the loveRais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amechaguliwa na wabunge wa...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

DA, ANC waridhia kuunda serikali ya mseto Afrika Kusini

Spread the loveChama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress, ANC,...

error: Content is protected !!