MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na wenzake watano, wamenusurika kifo baada ya kupata ajali maeneo ya Kilwa mkoani Lindi, akitokea Nanguruku alikokuwa anahutubia mkutano wa hadhara. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza na MwanaHALISI Online, leo Alhamisi, tarehe 16 Februari 2023, Mkurugenzi wa Habari CUF, Mhandisi Mohamed Ngulangwa, amesema ajali hiyo ilitokea jana Jumatano, majira ya saa 1.00 usiku, baada ya gari alilopanda Prof. Lipumba kupinduka.
Mhandisi Ngulangwa amesema, Prof. Lipumba alikuwa njiani kuelekea Kilwa Kivinje, kwa ajili ya maandalizi ya mkutano wa hadhara ulipangwa kufanyika leo.
Amesema wahanga wa ajali hiyo walipata majeraha madogo na kwamba walifikishwa hospitalini kwa ajili ya matibabu hivyo hali zao kiafya zinaendelea vizuri.
“Gari iliyopinduka haikuwa na tatizo, mwendo kasi haukuwa mkubwa lakini gari ilipinduka. Tunachoshukuru pamoja na kwamba gari iomeharibika vibaya lakini hakuna mtu aliyeumia sana ni majeraha madogo,” amesema Mhandisi Ngulangwa.
Alipoulizwa kama Prof. Lipumba ataweza kuhutubia mkutano wa hadhara wa leo, Mhandisi Ngulangwa amejibu akisema kwa sasa ni mapema mno kusema kama suala hilo litawezekana au lah, huku akieleza kwamba, kama itashindikana kuna uwezekano mkutano huo ukaahirishwa hadi kesho tarehe 17 Februari 2023.
Leave a comment