ALIYEKUWA Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Dk. Rugemeleza Nshala leo Alhamisi amehojiwa na katika Kituo cha Polisi Kanda Maalumu Dar Es Salaam kwa tuhuma za kutoa maneno yaliyosababisha taharuki kinyume na kifungu cha 63 C (i) cha kanuni ya adhabu. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Dk. Nshala ameitikia wito huo kwa mara nyingine baada ya juzi Jumanne kutohojiwa kutokana na askari aliyepangwa kumhoji kudaiwa kuwa amepata msiba.
Hata hivyo, Dk Nshala ambaye pia ni Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira (LEAT), ameieleza MwanaHALISI Online kuwa amepata dhamana baada ya Polisi kufanya kazi yao Kwa weledi mkubwa.
“Tumechelewa kutoka polisi kwa sababu nyaraka za wadhamini zilikuwa na kasoro. Nshala katoa maelezo ya jina lake, anuani na makazi tu. Mengine yote kasema atayaeleza mahakamani,” ameeleza Wakili wa Dk. Nshala, Hekima Mwasipu.
Tarehe 21 Julai Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai aliwaita baadhi ya watu kuhojiwa na polisi akidai kuwa walitoa maneno yenye viashiria vya uchochezi na matumizi ya lugha za kifedhuli kwa viongozi.
Miongoni mwa walioitwa kuhojiwa na Jeshi la Polisi ni Dk. Nshala, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, Wakili Boniphace Mwabukusi na Maluka Nyagali ‘Mdude Nyagali’.
Leave a comment