JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia watu wawili wanaotuhumiwa kuwapa dawa za kulevya wanawake bila kujijua kisha kuwapiga picha za utupu. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo tarehe 19 Disemba 2023 na Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, akizungumzia operesheni maalum ya kuwakamata wahalifu iliyoanza kufanyika Septemba mwaka huu.
Kamanda Muliro amesema watuhumiwa hao wamekamatwa wakiwa na vitu mbalimbali walivyoiba ikiwemo kompyuta mpakato (laptop) 10, simu za mkononi 305, televisheni 36, kamera 4 na makava ya simu 160.
“Katika maeneo mbalimbali jijini tumewanasa watuhumiwa wakiwemo watu wawili ambao majina yamehifadhiwa kwa sababu za uchuguzi. Huwatongoza wanawake, wanawawekea dawa za kuwalewesha, kuwafanyia vitendo vya udhalilishaji wa kingono na kuwapiga picha, kuwatishia kuwaua wakitoa siri za udhalilishaji huo na baadae kuwaibia simu, laptop na fedha,” amesema Kamanda Muliro.
Katika tukio lingine, Kamanda Muliro amesema watu watatu, Msabaha Michael, Juma Athumani na Joseph Januari, wanashikiliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano kufuatia tuhuma za wizi wa vifaa vya boti inayomilikiwa na raia wa Afrika Kusini, Van Baurenm.
Leave a comment