Thursday , 2 May 2024
Home Kitengo Biashara NMB yashinda tena tuzo ya kuongoza kuwafadhili wajasiriamali
Biashara

NMB yashinda tena tuzo ya kuongoza kuwafadhili wajasiriamali

Spread the love

Benki ya NMB imetunukiwa tena tuzo na jukwaa la kufadhili ujasiriamali duniani (SME Finance Forum) kutokana na huduma zake wezeshi na ufadhili wake wa kuendeleza biashara za wafanyabiashara wadogo na wakati nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Ushindi iliyoupata benki hiyo kwenye tuzo za mwaka huu za ufadhili wa ujasiriamali duniani (Global Finance Awards 2023 – GSMEFF 2023) ni wa Mfadhili wa Ujasiriamali wa Mwaka upande wa Afrika uliyoipa tuzo ya fedha.

Mkuu wa Idara ya Biashara wa Benki ya NMB, Alex Mgeni ( katikati ) katika picha ya pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la IFC aliemaliza muda wake, Matthew Gamser pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la IFC, Qamar Saleem, baada ya kupokea tuzo ya Mwezeshaji Bora wa Kifedha kwa Biashara Ndogo na za Kati (SMEs) katika bara la Afrika, kwa niaba ya Benki ya NMB.


Washindi wa tuzo za mwaka huu
walitangazwa wakati wa mkutano wa jukwaa hilo uliofanyika kati ya tarehe 12 na 14 Septemba huko Mumbai, India.

Kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake, tuzo za GSMEFF 2023 zinatambua dhamira na mafanikio ya taasisi za fedha na kampuni zinazojihusisha na teknolojia za huduma za kifedha (fintech) katika kuwahudumia wateja wao ambao ni wajasiriamali wadogo na wakati.

Ujumbe wa kauli mbiu ya tuzo za mwaka huu, ambayo ni “Mifumo ya Kidijitali na Mustakabali wa Ufadhili wa SMEs,” uliendana na dhamira ya NMB ya kuwasaidia wajasiriamali wadogo na wakati kwani ulizingatia jinsi mifumo ya kidijitali inavyogusa mabadiliko ya ukuaji wa uchumi duniani.

Akizungumzia ushindi wa tuzo ya mwaka huu, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, amesema heshima hiyo ni ushahidi mwingine wa juhudi za dhati za benki hiyo za kuziba pengo la kuwafadhili wajasiriamali nchini.

Mkuu wa Idara ya Biashara wa Benki ya NMB, Alex Mgeni (pili kulia) akipokea tuzo ya Mwezeshaji Bora wa Kifedha kwa Biashara Ndogo na za Kati (SMEs) katika bara la Afrika kwa Mwaka 2023 kutoka kwa Waziri wa Muungano wa Biashara Ndogo na za Kati wa Serikali ya India, Narayan Rane, katika hafla ya tuzo za Kimataifa za Mitaji kwa Biashara Ndogo na za Kati (Global SME Awards) iliyofanyika Jijini Mumbai, India mwishoni mwa wiki. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la IFC, Qamar Saleem na Kushoto ni Mkurugenzi wa Benki Kuu ya India, India Alok Kumar Choudhary.

“Tuzo hii kimsingi inathamini mchango na ushiriki wa benki yetu katika kuwafadhili wajasiriamali na uwekezaji inaoufanya katika uvumbuzi wa kidijitali,” aliongeza.

NMB inazingatia maendeleo ya wafanyabiashara haa kutokana na mchango wao mkubwa katika ujenzi wa taifa kwa kutengeneza ajira, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha mapato ya wananchi.

“Tuzo hizi na heshima tuliyopata ni ushahidi wa mwendelezo wa ubora wa huduma zetu na dhamira ya dhati ya ubunifu ya NMB,” amesema Zaipuna katika taarifa ya kuutangazia umma mafanikio hayo.

Huu ukiwa mwaka wake wa sita, tuzo za ufadhili wa ujasiriamali zilianzishwa mwaka 2018 na SME Finance Forum ambao ni mtandao wa taasisi za fedha wa kusaidia kuzikwamua kifedha biashara ndogo na za kati duniani.


Katika pongezi zake kwa washindi, Afisa Mtendaji Mkuu wake,
Matthew Gamser, alisema ushindani wa mwaka huu ulikuwa mkubwa kutokana na washiriki kuwa wengi wakitoka katika nchi nyingi ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Kwa upande wake, mtu anayetarajiwa kumrithi, Qamar Saleem, alisema kuwafadhili wajasiriamali ni zaidi ya kuwasaidia kifedha kwani kufanya hivyo pia kunabadilisha maisha ya watu wengi.

SME Finance Forum, inayoratibiwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) la Benki ya Dunia, ilianzishwa mwaka 2012 na nchi 20 tajiri duniani (G20) chini ya mwamvuli wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Ujumuishaji wa Kifedha (GPFI).

Majukumu yake makubwa ni pamoja na kusimamia wanachama wake kubadilishana maarifa, kuchochea ubunifu na kukuza ukuaji wa wajasiriamali.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Biashara

Cheza sloti ya Zombie Apocalypse na ushinde kirahisi

Spread the love Wengi wetu hupenda filamu za Mazombie huwa zinatishakidogo lakini...

Biashara

Ushirikishwaji wa wafanyakazi ni muhimu katika utekelezaji wa sera za afya na usalama kazini

Spread the love  KILA ifikapo Aprili 28 ya kila mwaka, dunia huadhimisha...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Oryx gesi yagawa mitungi, majiko 100 kwa waandishi wa habari Dar

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gesi Tanzania imegawa mitungi 100 ya gesi...

Biashara

Wazir Jr kinara wa ufungaji KMC FC ajiunga Meridianbet

Spread the love    MUITE Wazir Jr ‘The King of CCM Kirumba’,...

error: Content is protected !!