Thursday , 2 May 2024
Home Kitengo Biashara NMB yaazimia kushirikiana kimkakati na wanasheria
Biashara

NMB yaazimia kushirikiana kimkakati na wanasheria

Spread the love

BENKI ya NMB imeazimia kuwa na ushirikiano wa kimkakati na taasisi za kisheria nchini kutokana na umuhimu wa tasnia ya sheria katika maisha ya binadamu na maendeleo kwa ujumla. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

 Azma hiyo ilibainishwa rasmi mwishoni jana Jumamosi jijini Dar es Salaam katika mkutano maalumu wa kwanza kati ya benki hiyo na wanasheria binafsi.

Waziri wa Sheria na Katiba, Balozi Dk. Pindi Chana (katikati), akiwa ameshikana mikono na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Omary Said Shabaan (wa pili kulia) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wa pili kushoto), wakati wa hafla maalum iliyoandaliwa na Benki ya NMB iliyoikutanisha benki hiyo na Taasisi za Sheria Mkoa wa Dar es Salaam. Kushoto ni Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara Benki ya NMB, Filbert Mponzi na kulia ni Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam, Dismas Prosper.

 Akizungumza katika hafla hiyo iliyoaandaliwa kwa ajili ya wanasheria wa Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema mikutano kama hiyo ya kujengana na kubadilishana uzoefu itafanyika nchi nzima na itakuwa endelevu.

 “Lengo la mikutano hii ni kujenga na kudumisha mahusiano mazuri kati ya Benki ya NMB na wadau wa sheria na wanasheria binafsi nchini,” kiongozi huyo alisema na kusisitiza kuwa Taaluma ya Sheria ni miongoni mwa taalumu muhimu katika ujenzi wa taifa.

 “Sheria ina mchango mkubwa sana kwenye maisha ya kila siku ya mwanadamu, na hivyo basi ni taaluma ambayo kwa pamoja inatupasa kuilinda, na kuikuza,” aliongeza.

 Aidha, Zaipuna aliwaambia waliohudhuria hadhara hiyo kuwa sekta ya sheria pia ina mchango mkubwa katika ukuaji wa biashara na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Waziri wa Sheria na Katiba, Balozi Dk. Pindi Chana (kushoto), Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (katikati) Waziri wa Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Omary Said Shabaan (kulia) wakijadiliana jambo wakati wa hafla maalum iliyoandaliwa na Benki ya NMB iliyoikutanisha benki hiyo na Taasisi za Sheria Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa ni muendelezo wa ushirikiano baina ya pande hizo mbili.


Hiyo ni kupitia sheria, sera na kanuni bora za uwekezaji, umiliki wa vyanzo vya uzalishaji na utendaji wa kibiashiara vitu ambavyo ni moja ya misingi imara ya uchumi wa kiushindani na unaojitegemea.

Katika muktadha huo, Zaipuna aliishukuru Serikali kwa mageuzi chanya inayoendelea kuyafanya kuweka mazingira wezeshi ya kibiashara nchini ambayo yameifanya Tanzania kuorodheshwa kama nchi bora zaidi kwa vigezo vya uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mazingira hayo pamoja na mchango wa tasnia ya sheria yameiimarisha sekta ya kibenki nchini na kuifanya NMB kuwa na ufanisi mkubwa kihuduma na kiutendaji.

 “Tasnia ya sheria imeendelea kuwa na mchango mkubwa na muhimu sana katika sekta ya kibenki. NMB, tukiwa miongoni mwa taasisi kubwa zaidi za kifedha nchini Tanzania, tumekuwa bega kwa bega na taasisi za kisheria tukishirikiana kwenye masuala mbalimbali ya kibiashara.”

 Zaipuna alibainisha kuwa ushirikiano huo pamoja na mabadiliko makubwa ya kuitendaji iliyopitia NMB na uwekezaji katika mifumo, rasilimali watu na utawala bora, vimeiwezesha taasisi hiyo kuwa benki kubwa, imara na bora nchini.


 
Kwa sasa, NMB inayoongoza kwa faida nchini, inalihudumia taifa kupitia matawi zaidi ya 230, mawakala 24,000 na masuluhisho ya kidigitali kama NMB Mkononi.

 Mgeni rasmi wa shughuli hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Pindi Chana, aliipongeza benki hiyo kwa mtandao huo mpana ambao alisema umesaidia sana kupatikana kwa huduma za kifedha hata katika maeneo ya pembezoni mwa nchi.

 Waziri huyo alisema wazo la kukutana na kushirikiana kwa karibu na wanasheria ni ubunifu mkubwa unaostahili kuingwa na taasisi nyingine.

“Ushirikiano huu ni muhimu sana kwa maslahi mapana ya taifa hususani katika kuwahudumia wawekezaji ambao wanazidi kuongezeka kutokana na juhudi zinazofanywa na Serikali chini ya uongozi imara wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,” Dk. Chana alisisitiza.

Mkutano huo ulihudhuliwa pia na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Zanzibar, Bw Omar Said Shaaban, aliyesema mikutano ya aina hiyo pamoja na mada zilizotolewa na wataalamu kutoka TRA, Brela, Tume ya Madini na Kituo cha Uwekezaji Tanzania zitasaidia kuwajenga wanasheria kiutendaji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Equity Bank yaendelea kusotea mabilioni ya fedha mahakama rufani

Spread the loveBENKI za Equity ya Tanzania na Kenya, zimeendelea kupambana mahakamani...

Biashara

Cheza sloti ya Zombie Apocalypse na ushinde kirahisi

Spread the love Wengi wetu hupenda filamu za Mazombie huwa zinatishakidogo lakini...

Biashara

Ushirikishwaji wa wafanyakazi ni muhimu katika utekelezaji wa sera za afya na usalama kazini

Spread the love  KILA ifikapo Aprili 28 ya kila mwaka, dunia huadhimisha...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Oryx gesi yagawa mitungi, majiko 100 kwa waandishi wa habari Dar

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gesi Tanzania imegawa mitungi 100 ya gesi...

error: Content is protected !!