MATUMIZI ya Nishati jadidifu yatajwa kuwa chanzo kipya cha ajira kwa vijana nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Licha ya kuongeza ajira nchini nishati hiyo itachangia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Kampuni ya CSI Energy Group, Natacha Emilien akishukuru baada ya uteuzi huo na akitaja dira ya kampuni hiyo inayojihusisha na nishati.
“Nishati mbadala hunufaisha matabaka yote ya jamii kwa usawa zaidi, hasa wajasiriamali wadogo kutokana na upatikanaji wa nishati kwa bei nafuu, kutoa mafunzo.
“Pia inasaidia katika kushirikiana na wajasiriamali wanawake kama wakandarasi wadogo katika mnyororo wa thamani,”amesema Natacha.
Akizungumza katika kongamano la mjadala wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia uliofanyika jijini hapa Novemba 2022, Mkurugenzi wa Taasisi ya Climate Action Network Tanzania, Dk. Sixbert Mwanga alisema tafiti nyingi zinaonyesha Afrika ina kiwango kikubwa cha nishati safi inayotosheleza mahitaji ya wananchi wake.
Alisema nishati jadidifu ni chanzo kingine muhimu kitakachowezesha uzalishaji umeme bora kwa bei rahisi na kutosheleza mahitaji ya bara la Afrika.
“Nishati mbadala zilizopo ukifuatilia zinatosha na uzuri wa hizi hazihitaji kufuatwa na gridi ya Taifa, badala yake zenyewe ndiyo zinaifuata gridi ili ziende kufidia wengine wenye upungufu.”
Jitihada za Afrika katika nishati jadidifu
Wakati bosi wa CSI akitaja faida za matumizi ya nishati jadidifu kwa wananchi, Afrika miezi michache iliyopita imetoka kusaini mkataba wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (Irena) ambao utasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na uzalishaji wa nishati isiyo rafiki.
Oktoba 31, 2023 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko alitaja faida za mkataba wa Irene alipokuwa akiwasilisha azimio la mkataba huo bungeni jijini Dodoma.
Dk. Biteko alisema mkataba huo utasaidia kuimarika kwa mchango wa nishati jadidifu katika uzalishaji wa nishati ya umeme na kuliwezesha Taifa kuwa na vyanzo mchanganyiko vya umeme unaoendana na mahitaji ya ukuaji wa kiuchumi na kijamii, pia kutatua changamoto ya vyanzo vya umeme visivyo endelevu na uhakika.
Leave a comment