August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mume awafungia ndani mke, watoto kwa miaka 17

Spread the love

MWANAMKE wa Brazil amezungumzia masaibu yake ya kufungiwa – pamoja na watoto wake wawili – na mumewe kwa miaka 17, vyombo vya habari nchini humo vinaripoti.

Familia hiyo iliokolewa kutoka kwa nyumba hiyo katika kitongoji cha Guaratiba, magharibi mwa Rio de Janeiro siku ya Alhamisi, polisi walisema.

Mume aliyefungia familia yake kwa miaka yote hiyo amekamatwa.

Katika maoni kwa mamlaka yaliyonukuliwa na tovuti ya habari ya Brazil G1, mwanamke huyo alidai kuwa mumewe alisema angetoka nje ya nyumba hiyo tu atakapofariki dunia.

Kulingana na polisi, mwanamume huyo – aliyetajwa kama Luiz Antonio Santos Silva – na mkewe walikuwa wameoana kwa miaka 23.

Baada ya kuokolewa, inasemekana mama huyo aliambia mamlaka kwamba kuna wakati walikaa bila chakula kwa kwa siku tatu, na mara nyingi walinyanyaswa kimwili na kisaikolojia.

Nyumba walimofungwa pia ilikuwa mbovu, yenye mwanga mdogo na mazingira ya ndani ni machafu, picha zilizotolewa na polisi zinaonyesha.

Watoto hao wawili waliokomaa walikuwa wamefungwa kamba, ni wanyonge na wenye njaa walipopatikana, kulingana na polisi.

Wana umri wa miaka 19 na 22, ripoti ya vyombo vya habari vya ndani.

Kapteni William Oliveira wa kikosi cha kijeshi alisema katika maoni yaliyonukuliwa na gazeti la O Dia la Brazil kwamba awali alifikiri wawili hao walikuwa watoto kwa sababu ya kiwango chao cha utapiamlo.

‘’Tulipoona hali ya watoto hao wawili, tulidhani hawangenusurika kifo kwa wiki nyingine,’’ mkazi mmoja wa eneo hilo alisema.

Baada ya kuokolewa watatu hao walipelekwa hospitalini mara moja kutibiwa kutokana na upungufu mkubwa wa maji mwilini na utapiamlo, vyombo vya habari vya nchini vinaripoti. (Chanzo: BBC)

error: Content is protected !!