Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mbunge wa CCM aikosoa serikali ya JPM
Habari za SiasaTangulizi

Mbunge wa CCM aikosoa serikali ya JPM

Omar Mjaka Ali, Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Pemba Vitongoji alipokuwa anazungumza na wanaCCM. Picha ndogo Rais John Magufuli
Spread the love

MBUNGE mstaafu wa Chama cha Mapinduzi, Omar Mjaka Ali, amesema serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli inahitaji kuokolewa kwa sasa imepotea na kupoteza mwelekeo kutokana na rais kukosa washauri, anaandika Dany Tibason.

Mbunge huyo ambaye alikuwa mbunge wa CCM tangu mwaka 2000 hadi 2005 jimbo la Vitongoji kisiwani Pemba, amesema kuwa kwa sasa nchi haina mwelekeo kutokana na kuendeshwa kwa matamko na matakwa ya mtu mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari kutoka chama cha waandishi wa habari kutoka mkoa wa Dodoma (CPC) pamoja na wenyeji wa Chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Kusini Pemba (PPC) nje ya ofisi ya mkuu wa wilaya ya Chake Chake mbunge huyo mstaafu amesema kuwa kwa sasa taifa limekosa mwelekeo.

Katika ziara hiyo iliyofadhiliwa na Muungano wa vyama vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) alieleza kuwa yapo mambo mengi ambayo yanafanywa bila kufuata utaratibu na kuminya matakwa ya wananchi likiwemo suala la kutoonyesha vikao vya bunge moja kwa moja.

“Mimi nimekuwa mbunge wa CCM tangu mwaka 2000 hadi 2005 na mimi ni mwana CCM na nitaendelea kuwa CCM lakini yapo mambo mengi ambayo nayaona katika serikali ya Magufuli yakiwa siyo mazuri na hayo yanafanyika kutokana na kiongozi huyo kukosa washauri wazuri.

“Washauri wa rais wanashindwa kumweleza ukweli kuwa serikali ni ya wananchi, yapo mambo mengine ambayo wananchi wanayataka hata kama yeye hayataki mfano kitendo cha serikali kuzuia kuoneshwa kwa vikao vya bunge moja kwa moja, hiyo ni kuwaonea wananchi,” amesema mbunge huyo mstaafu.

Katika hatua nyingine, amekemea kitendo cha serikali kuwapora mali zao viongozi wastaafu na kudai kuwa jambo hilo siyo zuri kwani linaweza kusababisha migogoro ambayo siyo sahihi na kujenga chuki kati ya jamii na serikali.

Akizungumzia wajibu wa wabunge, amesema wote ni sawa wakiwa bungeni, awe CCM au Upinzani, hivyo wanatakiwa kutambua wajibu wao hususani katika kuisaidia serikali pale ambapo inaonekana kwenda tofauti.

Amesema kuwa wabunge wengi wamekuwa hawajui wajibu wao badala ya kuisimamania serikali wamekuwa ni watu wa kuijibia serikali au kujifanya wao ni sehemu ya serikali katika mambo ambayo ni ya msingi kwa maslahi ya jamii.

Aidha ameitaka serikali pamoja na bunge kuacha tabia ya kubeza maoni ya wapinzani badala yake maoni na ushauri wa wabunge wa upinzani yanatakiwa kufanyiwa kazi kwani kazi kubwa ya mbunge ni kuikosoa serikali ili iweze kukaa katika mstari.

“Mbunge ni mtu wa heshima iwe wa upinzani au wa chama tawala siyo jambo zuri kumtoa mbunge bungeni kwa kutumia jeshi la polisi kwa kufanya hivyo ni kumvunjia heshima mbunge na kulivunjia heshima bunge kwa ujumla hivyo washauri wanaomshauri rais na vyombo vyake wanatakiwa kutokuwa na hofu na badala yake wampe rais ushauri ambao ni sahihi
zaidi,” alisema Ali.

3 Comments

  • Kuwanyag’anya Viongozi mali, inategemea mali hizo wamezipataje. Kama wametumia madaraka yao kuiba mali za umma, lazima wanyang’anywe. Mwalim Nyerere angefanya hivyo hivyo. Wakati wa serikali ya tano, watu walijirundukia mali ambazo hawawezi kuelezea wamezipataje. Kama ni biashara basi waonyeshe kodi walizolipa, Na kama ni mishahara inajulikana. Sheria Hii inafanya ka ulimwengu muzima wizi ni kosa. China haunyang’anywi tu bali unafungwa hata kupigwa risasi. Nchi za Ulaya, utachunguzwa, na utapelekwa mahakamani kwa money laundering. Rais Magufuli hatuwa anazochukuwa zitawaudhi wezi na wadhurumaji. Ndiyo kuna makosa kwenye serikali yake, so far he is the best for Tanzania,

  • KAMA INGEKUWA KWA NIA NJEMA,HAKUNA AMBAYE ANGESEMA,WATU WANASEMA KWA SABABU HAKUNA NIA NJEMA NI VISA NA VISASI….KAMA KUNA NIA NJEMA MAKONDA ANA MAKOSA MANGAPI? ANA UTAJIRI WA KUTISHA WAKATI HAJAFIKISHA HATA MIAKA MITANO KWENYE UONGOZI,MENGI YAPO WAZI KABISA LAKINI YANAFUMBIWA MACHO,VIONGOZI WANGAPI WAMEJIMILIKISHA MALI ZA SERIKALI ? LAKINI WANAAMBIWA WAACHWE WAPUMZIKE….TUWE WAZALENDO TUSIWE MASHABIKI……..LA SIVYO YAFUKULIWE MAKABURI YOTE BILA KUBAGUA KIONEKANE KILA KITU KWA UWAZI

  • Tanzania ilikuwa imeoza, na vita hii siyo ya mtu mmoja. Rais Magufuli lazima anapata vitisho kutoka kwa watu mbali mbali, wengine wananguvu ya mali kushinda hata serikali. Watanzania wote wakimuunga mkono atakuwa na nguvu ya kuyafukuwa makaburi yote. Ndiyo kuna wengine anawafumbia macho, na wengi wezi wananchi wanawajuwa, lakini lazima aende pole pole, na pole pole ndiyo mwendo. Hakuna hata haja ya kusema wengine, hao ni marais wa zamani, katiba haumuruhusu kuwagusa, na ni katiba mbaya. Hawa watu wangetakiwa wapelekwe mbele ya sheria, kwani mali walizojirundikia ni za wananchi. Mpaka Tanzania impate katiba mpya watu kama hawa yatawakuta. Mugabe yamemukuta na umri wa miaka 93. Mali ya wizi huwezi kwenda nayo kaburini, utaiacha hapa hapa. kuhusu Makonda, utafika mwisho wake, atakitema alichokimeza kama ni cha wizi. Madaraka ya mwisho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!