April 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mbowe aumizwa na waliohamia CCM, awatahadharisha viongozi wapya

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa

Spread the love

FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amewashauri viongozi wa chama hicho, waliochaguliwa katika chaguzi zilizofanyika hivi karibuni, kutokuwa wabinafsi. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Mbowe ametoa ushauri huo leo tarehe 17 Desemba 2019, katika Kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Chadema, kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Kiongozi huyo wa Chadema amewaeleza viongozi hao kuwa, wamechaguliwa ili kulinda maslahi ya Chadema na si maslahi yao binafsi.

“Wamewaamini na kuwachagua kuwa wawakilishi wao, na sio mkajijenge binafsi. Wamewachagua kukijenga chama na si maslahi yenu binafsi. Nawapongeza sana, lakini zaidi nawapongeza nikitambua wajibu mzito ulioko mbele yetu,” amesema Mbowe. 

Wakati huo huo, Mbowe amezungumzia hatua ya baadhi ya viongozi wa Chadema, madiwani na wabunge waliokimbilia Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema kwamba chama chake kimejibu mapigo kuhusu hatua hiyo.

Mbowe amesema wakati CCM ikisuka mipango ya kuwanunua wabunge, madiwani na viongozi wake, Chadema ilijikita kusuka viongozi wapya, pamoja na kusaka wanachama wapya nchi nzima.

“Wako tuliokuwa nao miaka ya nyuma ambao nguvu iliwaishia katikati wakashuka kwenye treni, sisi tunasonga. Wakati watani zetu wanafanyabiashara ya madiwani na wabunge, sisi tulifanya kazi ya kuwaibua viongozi na wanachama kwa mamilioni nchi nzima,” amesema Mbowe na kuongeza;

“Ndoto za Rais John Magufuli kufikiria wanaweza kuiua Chadema, tumeijibu kwa hasira ya nguvu ya chama chetu.”

Aidha, Mbowe ameonya kwamba Chadema haitawafumbia macho watu watakaovunja umoja wa chama hicho, ingawa ameahidi kuwa hawatalipa kisasi kwa mabaya waliyofanyiwa.

“Hatutakubali yeyote atakayechezea chama chetu, hatutakubali kiongozi yeyote wa ngazi yeyote avunje umoja wetu. Hatutakubaliana na kiongozi yeyote wa nje ya chama atuchafulie umoja wetu. Wenzetu wa CCM wanaijadili Chadema kuliko wanavyojadili chama chao,” amesema Mbowe na kuongeza;

“Tunaweza kupoteza miaka mingi kulipiza kisasi,  kwa sababu tulifanyiwa mambo mengi mabaya, lazima tuweze kuuzidi ubaya. Tusikubali mioyo yetu kutawaliwa na chuki, hasira na visasi, tunapotafuta madaraka na mamlaka ya kuongoza nchi yetu, kusudio letu sio kuitenga Tanzania, ni kuwasaidia na kuwaunganisha Watanzania.”

error: Content is protected !!