October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Utabiri: Mvua kutikisa siku 5 mfululizo, mikoa 15 yatahadharishwa

Spread the love

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa utabiri wa Hali ya Hewa Hatarishi wa siku tano mfululizo, kuanzia tarehe 17 hadi 21 Desemba 2019, na athari zinazoweza kutokea kwenye mikoa 15 nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA, mikoa hiyo itakumbwa na mvua kubwa, zitakazosababisha athari mbalimbali. Pia, uwezekano wa mvua hizo kunyesha ni wa wastani.

Athari hizo ni pamoja na uharibifu wa mali na miundombinu, makazi ya watu kuzingirwa na maji, hatari ya maisha ya watu kutokana na maji yanayotiririka au maji ya kina kirefu, ucheleweshaji wa usafiri, na baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii kusimama.

Mikoa itakayo athirika ni, Dar es Salaam, Pwani, Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Ruvuma, Kisiwa cha Unguja na Pemba, Lindi, Mtwara, Morogoro, Tabora na Singida.

Mamlaka hiyo imetoa tahadhari ya mvua kubwa kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, kwa siku ya leo.

Pia, imetoa angalizo la mvua kubwa kwenye maeneo ya mikoa ya Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Morogoro na Kisiwa cha Unguja.

https://youtu.be/4_vaRGml-uU

Kesho tarehe 18 Desemba 2019, mamlaka hiyo imetoa angalizo la mvua kubwa kwenye maeneo ya Mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Ruvuma, Pwani, Dar es Salaam na Unguja.

TMA imetoa angalizo ya mvua kubwa inayotarajiwa kunyesha tarehe 19 Desemba mwaka huu,  kwenye maeneo ya Mikoa ya Mbeya, Lindi, Songwe, Iringa, Njombe, Ruvuma, Mtwara, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro maeneo ya Kusini.

Terehe 20 Desemba 2019 TMA imetoa angalizo kwamba mvua kubwa itanyesha katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Rukwa, Singida, Tabora, Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Pwani na Morogoro.

Wakati tarehe 21 Desemba 2019, mamlaka hiyo imetoa tahadhari ya mvua kubwa katika maeneo ya Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, ambapo uwezekano wa kutokea ni wa wastani huku kiwango cha athari zinazoweza kutokea kikiwa kikubwa.

Athari za mvua hizo zimeshaanza kuonekana jijini Dar es Salaam, ambapo leo baadhi ya wakazi wa jiji hilo shughuli zao za kijamii na kiuchumi zilisimama.

Huku baadhi ya barabara hasa ya Morogoro maeneo ya Jangwani, zikifungwa kutokana na kuzungukwa na maji yanayotiririka kwa kasi.

Wakati baadhi ya makazi hasa kwenye maeneo ya bondeni, yakiingia maji na kusababisha uharibifu wa mali.

error: Content is protected !!