KATIBU MKuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, anatarajiwa kushiki mafunzo kuhusu masuala ya uwazi na uwajibikaji, yaliyoandaliwa na Serikali ya Marekani kupitia mpango wa Program ya Uongozi ya International Visitor Leadership Program (IVLP). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Idara ya Mambo ya Nje, ACT-Wazalendo, Mwanaisha Mndeme, mafunzo hayo yanafanyika kuanzia tarehe 8 hadi 26 Aprili 2024, nchini Marekani.
“Dhima ya program ya IVLP ya 2024 inayoratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ni uwazi na uwajibikaji wa taasisi za umma. Ado atajumuika na washiriki wengine ambao ni viongozi kutoka taasisi zinazohusika na masuala ya uwazi na uwajibikaji kutoka nchi 24,” imesema taarifa ya Mndeme na kuongeza:
“Kwenye program hiyo, kwa kipindi cha wiki tatu, Ado na washiriki wengine watapata nafasi ya kupata uzoefu wa jinsi taasisi za Marekani zinazohusika na masuala ya uwazi na uwajibikaji zinavyofanya kazi.”
Chama cha ACT-Wazalendo ni miongoni mwa vyama vya siasa vya upinzani nchini Tanzania, vinavyosimamia masuala ya uwazi na uwajibikaji serikalini kupitia njia mbalimbali, ikiwemo uchambuzi wa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi wa Mahesabu ya Serikali (CAG) zinazotolewa kila mwaka, lengo ni kuonyesha maeneo yenye dosari na kisha kutoa mapendekezo juu ya namna ya kuboresha.
Pia, ACT-Wazalendo kimeunda Baraza Kivuli la Mawaziri linalosimamia utendaji wa Serikali wa kila siku, baada ya wapinzani kukosa uwakilishi wa kutosha bungeni.
Leave a comment