Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mapya yaibuka wamasai waliohamishwa Ngorongoro kwenda Msomera
Habari za SiasaTangulizi

Mapya yaibuka wamasai waliohamishwa Ngorongoro kwenda Msomera

Spread the love

MAPYA yameibuka kuhusu zoezi la Serikali kuwahamisha kwa hiari wamasai waliokuwa wanaishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kwenda maeneo ya Msomera mkoani Tanga, baada ya baadhi yao kudai kutolipwa stahiki zao kama walivyoahidiwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Madai hayo yameibuliwa hivi karibuni, wakati Serikali ikiahidi kukamilisha zoezi hilo Machi 2024. Awamu ya kwanza ilifanyika Juni 2022 ambapo kaya 551 zenye watu 3,010 na mifugo 2,521 zilihamishiwa Msomera nakupelekwa katika nyumba 503 zilizokuwa zimejengwa na Serikali.

Ngorkisho Lowassa Songopa, mama mwenye watoto wanne (wa kiume watatu na wa kike mmoja), ametoka hadharani na kudai kuwa Serikali ilimuahidi kumpatia nyumba tano kwa ajili yake na watoto, pamoja na fedha za kujikimu akiwa Msomera, lakini imepita miezi miwili bila ahadi hiyo kutekelezwa.

“Tuliambiwa tutaenda kupewa nyumba tano lakini mpaka leo hatujapewa, watoto wangu wa kiume wako watatu na mwanamke mmoja lakini watoto wa kiume hadi leo hawajaletwa Msomera nimekuja mimi na binti yangu na tumepewa nyumba moja ndio tukaa haina kitanda tunalalia kwenye godoro sababu fedha hatujapewa hadi leo,” alidai Songopa na kuongeza:

“Tangu tumeletwa hapa imefunguliwa akaunti lakini hatujapewa fedha hadi leo, kama mnavyoona nalala chini na watoto wadogo sababu hatuna fedha ya kununua vitanda. Nakosa chochote cha kula sababu hata mahindi waliyotupa tunashindwa kusaga sababu hatuna hela na hata shamba tulililopewa la heka 2.5 tumeshindwa kulima sababu hatuna hela.”

Katika hatua nyingine, kwa mujibu wa baadhi ya wamasai hao, wanadai walipokuwa wanahamishwa Ngorongoro kwenda Msomera waliambiwa kuna huduma zote za msingi za kijamii, ikiwemo za afya na maji safi na salama, lakini walipofika wamekuta hazipo.

“Tuliambiwa kuna huduma za afya lakini si kweli, mtu akiumwa ili kwenda kufuata hospitali inatakiwa upande pikipiki kwa gharama ya 20,000 ili upelekwe hospitali, maisha ya huku ni magumu sana na pia tuliambiwa maji yapo lakini hakuna na hata kidogo yanayoletwa ni ya chumvi sana,” alidai mwananchi mmoja.

Baada ya kuibuka kwa madai hayo, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kupitia kwa Kaimu Meneja-Uhusiano wa Umma, Hamis Dambaya, imetoa ufafanuzi ikisema Songopa alilipwa stahiki zake zote pamoja na za wategemezi wake, ambapo tarehe 16 Januari 2024 walisaini malipo ya fidia ya maendelezo na motisha na waliondoka Ngorongoro siku mbili baadae.

“Wakati wa zoezi la uthamini, kusaini na kuhama kukamilika, stahiki zake za malipo ya fidia zilihusisha nyumba nne, mazizi mawili pamoja na motisha ambayo mamlaka ilimlipa mkuu wa kaya fedha hizo kupitia akaunti namba yake ya benki,” imesema taarifa ya NCAA na kuongeza:

“Wakati wa zoezi la uthamini, kaya hiyo ilikutwa na msimamizi mmoja wa kaya ambaye ni Songopa na sio kaya tano kama ilivyoelezwa kwenye video na ndio maana hata walipofika Msomera walikabidhiwa nyumba moja.”

Mara kadhaa serikali imekuwa ikikanusha madai hayo kwamba Msomera hakuna huduma za msingi na au kuna vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, ambapo Msemaji wake mkuu, Mobhare Matinyi mara kadhaa alinukuliwa na vyombo vya habari akisema katika kutekeleza zoezi hilo imekua ikizingatia haki za wananchi ikiwa sambamba na kuwapa bure vitu vya kuwashawishi.

Miongoni mwa vitu ambavyo Serikali inasema imewapatia watu hao ni nyumba yenye vyumba vitatu vya kulala na eneo lenye ukubwa wa eka 2.5 lenye hati yake na mwananchi mwenye mifugo anapewa eka 5.

Pia, Matinyi alisema Serikali imeweka mazingira mazuri ya ufugaji ikiwemo kujenga mabwawa ya maji na kuchimba visima kwa ajili ya wananchi kupata huduma ya maji. Pia, alisema kila mwananchi aliyekubali kuondoka analipwa fidia ya Sh. 10 milioni.

1 Comment

  • Neno la wafugaji dhidi ya neno la serikali. Malalamishi haya ni ya kwanza kuyasikia. Kumbe serikali inawalipa hadi milioni 10, mbona hawasemi ?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za SiasaTangulizi

Samia awataka watanzania kudumisha muungano

Spread the loveRais wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuendeleza Muungano kwa...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

error: Content is protected !!