March 7, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Makontena ya Makonda kugaiwa kwa umma

Spread the love

IWAPO Makontena 20 ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda yanayopigwa mnada na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kupitia Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart yatakosa mnunuzi, yatagaiwa kwenye taasisi za umma. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Leo tarehe 15 Septemba 2018 makontena hayo yalipigwa mnada kwa mara ya nne mfululizo na kukosa wanunuzi, kutokana na wateja waliohudhuria kwenye mnada uliofanyika bandarini jijini Dar es Salaam, kushindwa kufika bei elekezi.

Makontena hayo 20 yenye samani mbalimbali ikiwemo meza na viti vya ofisi, yanapigwa mnada baada ya kukwama bandarini kutokana na kudaiwa kodi ya kiasi cha Sh. 1.2 bilioni. Na kwamba TRA imepanga bei elekezi kwa kila kontena kuwa ni Sh. 60 milioni ili kufidia deni hilo.

Kwa mujibu wa Kamishna wa TRA,Charles Kichere amesema kuwa, bei elekezi ya makontena hayo haitaweza kupungua kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Forodha ya Afrika Mashariki, kama baadhi ya wateja wanavyopendekeza.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, Kamishna Kichere ameeleza kuwa, endapo wanunuzi hawatafika bei elekezi, sheria inaelekeza kuwa, makontena hayo yagaiwe kwenye taasisi za umma.

“Bei inapangwa kwa mujibu wa sheria, kabla ya bei kupangwa hesabu hukokotolewa ikiwemo ushuru wa forodha na gharama za kuhifadhi mizigo. Sheria ya Ushuru wa Forodha ya Afrika Mashariki inaelekeza jinsi ya kukokotoa bei elekezi,” amesema na kuongeza Kamishna Kichere.

“Bei ya makontena iliyopangwa haiwezi kupunguzwa kwa mujibu wa sheria, na kama yakikosa wateja kuna utaratibu wake unaofuata. Inawezekana yakagaiwa katika taasisi za umma au kwenye huduma za kijamii.”

error: Content is protected !!