Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Tanzania haitegemei kuzalisha umeme kwa kutumia maji pekee bali inaendelea kuweka mkazo katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati nyingine kama gesi na jua ili kuwa mzalishaji mkubwa na nishati hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo tarehe 20 Septemba 2023 wakati akifungua Kongamano la Tano na Maonesho ya Nishati Tanzania na kupata maelezo kuhusu utayari wa Benki ya NMB kuwekeza kwenye maendeleo ya nishati.
Majaliwa baada ya kufungua kongamano hilo la siku mbili linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam, ametembelea banda la Benki ya NMB na kupata maelezo kutoka kwa Meneja Mwandamizi Idara ya Wateja Wakubwa upande wa Nishati wa NMB, Hamis Njapuka, kuhusu utayari wa benki hiyo kuwekeza kwenye maendeleo ya nishati.
“Tunaendelea na utafutaji wa gesi, tunataka tuwe wazalishaji wakubwa wa nishati, tuwe na umeme wa kutosha utakaopatikana kwa urahisi na nafuu na ziada tutauza nje ya nchi,” amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu amesema katika kongamano hilo la kimataifa la nishati ambalo limehusisha viongozi na wadau kutoka katika mataifa mbalimbali duniani litajadili namna bora ya kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa nishati.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema wameendelea kutekeleza mipango mbalimbali waliojiwekea katika kuhakikisha umeme unapatikana wakati wote nchini.
Dk. Biteko amesema zaidi ya kampuni 100 za nishati kutoka katika maeneo mbalimbali duniani zinashiriki katika kongamano hilo ambalo lilitanguliwa na mkutano wa viongozi wa nishati.
Leave a comment