Thursday , 2 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Majaliwa adaiwa kuwakimbia Malaigwanani Ngorongoro
Habari za SiasaTangulizi

Majaliwa adaiwa kuwakimbia Malaigwanani Ngorongoro

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa anadaiwa kuwakimbia viongozi wa kimila wa Kimasai wanaoishi wilayani Ngorongoro na badala yake kufanya kazi na wenzao wa wilayani Arusha, katika mgogoro unaofukuta kati ya serikali na jamii hiyo ya wafugaji. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).

“Sisi hatukualikwa kwenye mkutano wake (waziri mkuu Majaliwa) na wanaoitwa viongozi wa Malaigwanani na hivyo, siyo sehemu ya waliopitisha azimio la kututaka kuhama kwenye maeneo yetu ya asili na kuhamia kwingine,” ameeleza mmoja wa viongozi wa kabila hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Morindati.

Naye Mwenyekiti wa Malaigwanani wilaya ya Ngorongoro, Metui Ole Shaduo, amesisitiza kuwa wananchi wanaoishi maeneo ya hifadhi hiyo, hawako tayari kuondoka kwa kuwa walihamishwa zaidi ya mara moja.

Anasema, kabla ya kuhamishiwa Ngorongoro mwaka 1959, walikuwa katika Hifadhi ya Serengeti, ambapo wakati wanaondolewa waliambiwa hawataondolewa tena katika eneo walilohamishiwa.

Anasema, kitendo cha serikali kuwatumia Malaigwanani wanatoka nje ya wilaya hiyo na kuwaacha wenyeji halisi, hawawezi kukikubali na hivyo, yeye na wenzake wataendelea kupigania maslahi ya wananchi wao hadi mwisho.

Kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja siku mbili baada ya mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongella, kueleza kuwa jukumu la kualika wajumbe waliohudhuria mkutano kati ya viongozi hao wa kimila na waziri mkuu, halikuwa la ofisi yake.

Amesema, Malaigwanani wana utaratibu wao wa kualikana wenyewe na kwamba utaratibu huo unajulikana.

Kwa takribani miezi mitatu sasa, kumekuwa na mgogoro kati serikali na jamii ya wafugaji wanaoishi katika hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha.

Kiini cha mgogoro wa sasa, kinatokana na hatua ya serikali ya kutaka kuwahamisha wafugaji kutoka maeneo ya hifadhi na kuwapeleka katika maeneo mengine, ikiwamo Simanjiro mkoani Manyara na Kilindi, mkoani Tanga.

Baadhi ya wafugaji wamekuwa wakipinga uhamisho huo, kwa maelezo kuwa wamekuwapo katika eneo hilo kwa miaka nenda rudi na kwamba hakuna athari yoyote inayopatikana kwa hifadhi, kutokana na wao kuishi maeneo hayo.

Ni kufuatia mgogoro huo, Rais Samia Suluhu Hassan, aliamua kumuagiza waziri wake mkuu, kufuatilia kwa karibu jambo hilo na kisha kumpa taarifa.

Aidha, katika siku za karibuni, kumedaiwa kujitokeza watu walioghushi majina wakionekana wamekubaali kuhama kwenye Hifadhi ya Ngorongoro kwa hiari, jambo ambalo linapingwa na baadhi ya viongozi wa kimila wa kabila la wamasai.

Viongozi hao wa kimila – Malaigwanani – wanadai kuwa hawakushirikishwa katika mchakato wa kuwahamisha kutoka Ngorongoro na hivyo, kilichotendeka katika mkutano kati ya waziri mkuu na wanaoitwa viongozi wa kimila, hakiwahusu na hawakibariki.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella

Akizungumzia sakata hilo, Mongella anasema, “kama kuna watu wana ushahidi wa jambo hili, naomba waulete ili serikali iweze kuufanyia kazi na ukweli kujulikana.”

 Aliongeza, “kama wanaona kwenye orodha iliyopo, huyu sio mwenzao, wanapaswa kutoa taarifa ili serikali iweze kuchukua hatua. Tunataka wao wenyewe wasimamie jambo hili kwa kuwa ni shirikishi.”

Kwa mujibu wa Mongella, kuna timu maalumu iliyoundwa kwa ajili ya kusajili watu wanaotaka kuhama kwa hiari, na kwamba hufanyika uhakiki wa kuthibitisha iwapo walioandikishwa ni wakazi halisi wa maeneo hayo ya hifadhi.

Mkuu huyo wa mkoa amesema, zoezi la kuwahamisha wananchi wanaoishi Ngorongoro ni la hiari na kwamba Serikali inaliendesha kwa mujibu wa sheria na misingi ya utawala bora.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

Habari za Siasa

Mavunde aomba bilioni 231.9 bajeti wizara ya madini

Spread the loveWAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde leo Jumanne amewasilisha hotuba ya...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu amjibu Fatma Karume kuhusu Rais Samia

Spread the love  MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Slaa: Watanzania iungeni mkono Chadema uchaguzi 2025

Spread the loveMWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Dk. Wilbroad Slaa, amewataka watanzania wakiunge...

error: Content is protected !!