Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Maalim Seif kuhamia ACT; Samani za CUF Unguja, Pemba ‘zatekwa’
Habari za SiasaTangulizi

Maalim Seif kuhamia ACT; Samani za CUF Unguja, Pemba ‘zatekwa’

Spread the love

UAMUZI wa Maalim Seif Shariff Hamad, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) kuhamia Chama cha ACT-Wazalendo umekwenda sambamba na kubebwa kisha kutokomea kwa samani zilizokuwepo kwenye Makao Makuu ya Ofisi ya CUF, Mtendeni visiwani Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Kwenye ofisi hizo tayari samani mbalimbali zimetolewa ikiwemo meza, viti na vitu vingine vilivyokuwa vikitumika kwenye ofisi hiyo kabla ya Maalim Seif kutangaza kuhamia ACT-Wazalendo.

“Hakuna CUF tena hapa, kama Maalim Seif si kiongozi CUF maana yake hapa hakuna chama tena. Hivi vitu viliwekwa na wenye mapenzi na chama hivyo, acha virejee kwa wenyewe,” ameeleza Kombo Juma Kombo, Mkazi wa Unguja akiwa kwenye eneo la tukio.

Amesema kuwa, Maalim Seif ndiye aliyekijenga chama kwa jasho lake, kuondoka kwake ndio kuondoka kwa Wazanzibari wote kwenye chama hicho.

Hata hivyo, taarifa kutoka Pemba zinaeleza kuwa, baadhi ya ofisi zilizokuwa zikitumiwa na CUF zimebadilisha na kupakwa rangi ya bendera ya ACT-Wazalendo.

Akiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari leo tarehe 18 Machi 2019, Maalim Seif amesema “…lakini nikufahamishe, ofisi nyingi ni majengo binafsi ya watu kama wataridhia wayachukue.”

Kwenye mkutano huo Maalim Seif amesema, yeye, waliokuwa viongozi wa CUF pamoja na wanachama wanaomuunga mkono, wanahamia ACT-Wazalendo.

Uamuzi huo umekuja saa chache baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutoa hukumu katika kesi Na. 23/2016 kwamba, Prof. Ibrahim Lipumba ndio mwenyekiti halisi wa CUF.

Maalim Seif ameeleza kuwa, walifungua kesi hiyo ili kupinga uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia uamuzi wa ndani ya CUF pale alipotangaza kumtambua Prof. Lipumba kama mwenyekiti licha ya kujiuzulu.

Amedai, hatua hiyo ni muendelezo wa mpango wa dola kwa lengo la kuhujumu na kuidhoofisha CUF na kuihujumu demokrasia nchini.

Kutokana na hivyo, yeye na wanamuunga mkono wameona njia sahihi ni kutafuta jukwaa lingine la kuendeleza mapambano ya kisiasa waliyokuwa wanasimamia wakiwa CUF.

Maalim Seif amesema, jukwaa sahihi walilochagua kulitumia kwa kuelekeza nguvu zetu zote ni chama cha ACT-Wazalendo, hivyo hawatakubali kupanda na kushuka mahakamani huku wakishindwa kufanya shughuli za kisiasa.

“Labda lengo ni kutufanya tuendelee kupanda na kushuka mahakamani huku tukishindwa kufanya shughuli za kisiasa. Sasa imetosha.

“Mapambano ya kisiasa lazima yaendelee. Kwa msingi huo, mimi na wenzangu katika uongozi tumetafakari kwa kina juu ya upi uwe mwelekeo wetu iwapo maamuzi ya kesi yangekwenda hivi yalivyokwenda,” amesema Maalim Seif na kuongeza;

“Tumeona njia sahihi ni kutafuta jukwaa lingine la kuendeleza mapambano ya kisiasa tuliyokuwa tukiyasimamia kupitia CUF. Jukwaa tuliloamua kulitumia kwa kuelekeza nguvu zetu zote ni Chama cha Alliance for Change and Transparency – ACT – Wazalendo.”

Maalim Seif ameeleza kuwa, wanahitaji jahazi la kuwafikisha kwenye Tanzania mpya inayoheshimu utu, ubinadamu haki na yenye neema inayofikia wananchi wote. “Jahazi hilo ni ACT-Wazalendo.”

Maalim Seif amesema, pamoja na kuamua kulitumia jukwaa la ACT-Wazalendo bado wanaamini ushirikiano katika vyama vyote.

“Niwahakikishie kwamba, bado tunaamini katika ushirikiano wa vyama vyote makini vya siasa na makundi mengine ya kijamii katika mapambano yetu ya kuleta demokrasia na haki nchini,” amesema na kuongeza;

“Umma haujawahi kushindwa popote duniani. Ndivyo historia inavyoonesha kote. Hatuna wasiwasi kwamba Umma wa Watanzania nao utashinda. Kauli yangu kwa wana-CUF wote wanaotuunga mkono na Watanzania wote kwa jumla ni kwamba wakati ni huu, wakati ni sasa. ShushaTangaPandishaTanga, safari iendelee.”

Leo Mahakama Kuu, Kanda Maalum ya Dar es Salaam imetoa uamuzi kwamba, Prof. Lipumba ndio mwenyekiti halali wa CUF.

“Nimeridhika na hiki ambacho kimetolewa ndani ya kiapo cha mjibu maombi namba moja (msajili wa vyama saisa) kwamba, kama hana mamlaka ya kukifuta chama basi hana mamlaka ya kumrejesha Profesa Lipumba kwenye kiti chake,” amesema Jaji Benhajj Masoud wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kuongeza;

“Msajili wa vyama vya siasa haishii kusajili chama tu, ndio maana sheria imempa mamlaka ya kufuta chama hivyo basi anamamlaka hayo.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!