Friday , 3 February 2023
Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Lissu atia mguu Chato

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti Chadema
Spread the love

 

ALIYEKUWA mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, Tundu Lissu amejitosa kwenye mjadala wa kuundwa kwa mkoa mpya wa Chato. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mjadala huo umetibua hali ya hewa nchini Tanzania, kutokana na mitazamo tofauti, baadhi wakitaka uruhusiwe kuwa mkoa, wengine wakipinga kwa hoja kwamba hauna vigezo.

Katika maoni yake kuhusu mjadala huo, Lissu ameungana na mtaalam wa makazi na Waziri wa zamani, Profesa Anna Tibaijukana ambaye amesema pasi na shaka kuwa Chato haina hadhi ya kuwa mkoa.

Wengine waliopinga pendekezo hilo kwa hoja ni pamoja na Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki Ngara, mkoani Kagera na Askofu wa Kanisa la Kiinjiri la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk. Benson Bagonza.

Wadadisi wa mambo wamelieleza Gazeti la kila siku la Raia Mwema kuwa mao ni ya Profesa Tibaijuka, Askofu Bagonza na Askofu Bagonza, yamemweka njiapanda Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, mwenye mamlaka ya mwisho kuamua hoja hiyo.

“Inawezekana Rais Samia anatamani sana kuona anatimiza ndoto ya mtangulizi wake kama alivyoahidi kuendeleza miradi aliyoanzisha Magufuli, lakini upande wa pili anashinikizo kubwa la maoni ya wananchi kwamba Chato haina hadhi, Hapo amewekwa njiapanda, anahitaji busara sana kuamua,” alisema mmoja wa makada wa CCM ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.

Chato ni mahali alipozaliwa Hayati John Pombe Magufuli, rais wa awamu ya tano aliyetutoka ghafla tarehe 17 Machi 2021.

Mchakato wa kuifanya Chato kuwa mkoa, ulianzishwa na Hatati Rais John Pombe Magufuli, mwenyewe na hivi sasa mjadala wa kutimiza ndoto yake, umeonekana kuligawa taifa.

Tayari mgawanyiko umeanza kuonekana kati ya Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Geita (RCC) na Baraza la Madiwa ni la Geita.

Prof. Anna Tibaijuka, aliyekuwa Mbunge wa Muleba Kusini

Wiki iliyopita RCC, ilipitisha pendekezo la kuundwa kwa mkoa mpya wa Chato, lengo likiwa kutaka kutimiza ndoto za Magufuli, lakini Baraza la Madiwani limepinga.

Akizungumza na Raia Mwema katika mahojiano maalum, Lissu alisema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana mamlaka, kwa mujibu wa Katiba ya nchi ya kugawa nchi katika mikoa na wilaya.

Lissu ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema taifa, alisema kipindi chote cha nchi yetu kuwa chini ya mfumo wa kikatiba na kiutawala wa urais, marais wetu isipokuwa John Pombe Magufuli, waligawa nchi katika mikoa na wilaya mbali mbali.

“Inaelekea Rais Magufuli naye alikuwa na lengo la kutumia mamlaka yake hayo ya kikatiba kutengeneza Mkoa Mpya wa Chato.

“Tofauti pekee ya Magufuli na marais wetu wote waliomtangulia ni kwamba, Magufuli alitaka kugeuza kijiji chake alikozaliwa kuwa makao makuu ya mkoa wa Geita ulioanzishwa mwaka 2012.

“Lengo hilo liliposhindikana, kwa sababu Chato haikuwa na bado haina hadhi ya kuwa makao makuu ya mkoa, Rais Magufuli akaamua kuunda mkoa mpya ambao ungetekeleza ndoto yake ya kijiji chake kuwa makao makuu ya mkoa.

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti Chadema

“Hii ndio sababu ya upendeleo mkubwa wa miradi ya maendeleo na miundombinu iliyojengwa Chato katika miaka mitano ya utawala wa Magufuli,” alisema Lissu.

Lissu ambaye hivi sasa anaishi uhamishoni baada ya kukimbia nchi kwa madai ya usalama wake, alisema “kwa hiyo, kama ni mfano wa matumizi mabaya ya madaraka ya Rais ya kugawa mikoa na wilaya, basi ni haya yaliyofanyika Chato kwa miaka mitano ya Magufuli.”

Mwasiasa huyo alimpa angalizo Rais Samia kuwa kama ni mfano wa kwanza wa matumizi mabaya ya madaraka yake ya urais itakuwa ni kwa yeye kubariki na kutekeleza ndoto hizo za Rais Magufuli za kuunda Mkoa wa Chato na kugeuza kijiji chake kuwa makao makuu ya Mkoa.

“Endapo Rais Samia atafanya hivyo, atakuwa amejifunga goli la bure yeye mwenyewe,” alisema Lissu.

Lissu alisema kama kuna sehemu ya mabadiliko ya Katiba yanayohitajika, eneo hili ni mojawapo ya mambo yanayopaswa kufanyiwa marekebisho.

Alisisitiza kuwa marekebisho ya Katiba katika eneo hilo ni jambo muhimu ili masuala ya kugawa maeneo yanatakiwa kufanywa na wananchi wenyewe kwa sababu ya mahitaji yao na sio kwa sababu ya mahitaji ya watawala.

1 Comment

  • Binafsi nimesoma maoni yote ya wanasiasa, wataaluma na viongozi wa dini lakini wengi wamejikita kutoa maoni yenye mchanganyiko ndani yake yaani. Baadhi ya maoni yamekuwa na mihemko ya ukosoaji wa utawala wa awamu ya tano na mengine yamegusa utaalamu na vigezo vya kuteua au kugawa mikoa. Binafsi naona suala la kugawa mkoa lingeangalia namna ya kusogeza huduma za jamii karibu na wananchi. Chato inaweza kuwa mkoa ila makao makuu yanaweza kupelekwa hata eneo la Nyakanazi yaani Wilaya ya Biharamulo ili kuwasogezea wananchi wa wilaya kama Kakonko (Kigoma) ambao kiuhalisia wanapata taabu kupata huduma kutoka manispaa ya Kigoma/Ujiji. Naweza pia kukosoa baadhi ya maoni ya wanasiasa yamesukumwa na suala la mikoa ya Geita na Kagera kukosa mapato endapo mikoa hiyo itagawanywa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Kamati ya Bunge yaitaka Serikali kuchunguza dawa za asili

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo...

Habari za Siasa

Kada NCCR-Mageuzi aliyepotea aokotwa porini akiwa taabani, hajitambua

Spread the love  MWENYEKITI wa Jumuiya ya Vijana ya Chama cha NCCR-Mageuzi,...

Habari za Siasa

ACT Wazalendo yataka Jaji Mkuu, Jaji Biswalo wajiuzulu kupisha uchunguzi fedha za Plea Bargaining

Spread the love  CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimemtaka Jaji wa Mkuu wa Tanzania,...

Habari za Siasa

Kigogo ACT-Wazalendo: Vyama vya upinzani vilikosea kumpokea Membe, Lowassa

Spread the love  KATIBU Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, amesema...

error: Content is protected !!