Friday , 3 February 2023
Home Gazeti Habari Mchanganyiko Takukuru yamkalia shingoni Kakoko wa bandari
Habari MchanganyikoTangulizi

Takukuru yamkalia shingoni Kakoko wa bandari

Injinia Deusdedit Kakoko
Spread the love

 

MKURUGENZI mpya wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Salum Hamduni, amemalizia kazi ya kuchunguza ubadhilifu wa mabilioni ya shilingi, ndani ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA). Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Taarifa kutoka ndani ya Takukuru zinasema, timu maalum iliyokuwa inafanyia kazi suala hilo, tayari imekamilisha kazi yake na muda wowote kutoka sasa, “mambo yatakua hadharani.”

Tuhuma za ubadhirifu wa mabilioni hayo ya shilingi, unamkabili aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko.

Uchunguzi dhidi ya Mhandisi Kakoko, unafanyika kufuatia Rais wa sasa wa Jamhuri, Samia Suluhu Hassan, kuamuru kumsimamisha kazi na kisha kuagiza kufanyika uchunguzi dhidi ya bosi huyo wa bandari.

Kakoko anakabiliwa na lundo la tuhuma, ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka, uzembe na ufujaji wa mabilioni ya shilingi, ambazo ni mali ya mwajiri wake.

Kakoko alikamatwa mkoani Morogoro, wakati akitokea mjini Dodoma. Amehojiwa kwa siku kadhaa na vigogo wa taasisi hiyo na vyombo vingine vya dola, kisha kuachiwa kwa dhamana.
Aidha, taarifa zinasema, watu wengine kadhaa, wakiwamo wasaidizi wake na mmoja wa wamiliki wa vyombo vya habari vilivyokuwa vinapigia chapuo serikali ya awamu ya tano, nao walihojiwa.

Mbali na hao, watoa huduma na wakandarasi kadhaa wa TPA, wamehojiwa na wanaendelea wanaochunguzwa na Takukuru.

Rais Samia, tayari amemteuwa Erick Hamis kuchukua nafasi ya Kakoko.

Mtoa taarifa wa MwanaHALISI Online amesema, suala la Kakoko, ni miongoni mwa mambo ambayo mkurugenzi mpya wa Takukuru, angependa kumalizana nalo mapema.

“Miongoni mwa mafaili ambayo mkurugenzi mpya (Kamishna wa Polisi (CP), Salum Hamduni, amekabidhiwa na mtangulizi wake, Brigedia Jenerali John Mbungo, na ambalo angependa kulimazana mapema, ni suala Kakoko,” ameeleza mmoja wa maofisa wa Takukuru ambaye hakupenda kutajwa jina lake.

Salumu Hamduni mkurugezni mkuu wa TAKUKURU

Ameongeza, “hivi tunavyozungumza, tayari kuna hatua kadhaa zimefikiwa, ambazo zinatoa sura mzuri la suala hilo. Hata nyaraka mbalimbali zilizosheni taarifa kuhusu tuhuma hizi, nyingi zimeshapitiwa.”

Hata hivyo, Hamduni ambaye ni mtu aliyebobea katika masuala ya uchunguzi amesema, “bado tunaendelea kuchunguza suala la Kakoko, ingawa tayari tumefika katika hatua nzuri na kwamba muda si mrefu, tutatoa taarifa kwa umma.”
Amesema, uchunguzi ni mchakato na utararibu ni kwamba sisi tukimaliza tunapeleka jalada kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kabla ya kwenda mahakamani.

Hamduni amegoma kuzungumzia kauli ya Brigedia Jenerali Mbungo, aliyesema kuwa Takukuru wamekamilisha kila kitu kwa asilimia kubwa na pale paliposalia, pamebaki mikononi mwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), Charles Kichere.

Akizungumza wakati wa kupokea ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Rais Samia aliagiza ofisi ya mdhibiti huyo wa fedha za umma, kufanya uchunguzi katika taasisi hiyo, kutokana na kuwapo kwa taarifa ya upotevu wa mabilioni ya shilingi.

Alisema, “…katika ripoti yako (CAG) kuna ubadhirifu mkubwa, uliofanywa katika shirika la bandari (TPA). Naomba Takukuru, hii ni special kazi (kazi maalumu), kashughulike.

“Najua kulikuwa na kamati iliundwa na waziri mkuu na wakafanya uchunguzi kidogo na hatua chache zilichukuliwa. Ni imani yangu, kuwa kama kuna ubadhirifu ndani ya shirika na kwa ripoti ile uliyonikabidhi jana jioni, kwamba kuna ubadhirifu kama wa Sh. 3.6 bilioni, karibu Sh. 4 bilioni.”

Kakoko anatuhumiwa kutaka kuhamisha kiasi kikubwa cha fedha za TPA, kutoka Benki kuu ya taifa (BoT), kwenda benki ya National Microfinance Bank (NMB), katika kipindi ambacho taifa lilikuwa kwenye msiba wa Dk. Magufuli.

Fedha hizo za umma, zilihamishwa siku tatu kabla ya mwili Dk. Magufuli kuzikwa, kijijini kwake, Rubambangwe, wilayani Chato, mkoani Geita Chato; na saa 72 baada ya kufariki dunia.

Dk. Magufuli alifariki dunia tarehe 17 Machi 2021, katika hospitali ya Mzena, mkoani Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizopo, fedha kutoka BoT kwenda NMB, zilihamishwa kwa mafungu manne na kupitia akaunti za dola za Marekani na shilimgi ya Tanzania.

Kiasi cha fedha ambacho kilihamishwa kutoka BoT kwenda NMB, ni dola za Marekani 11, 799,357.91 pamoja na Sh. 6.3 bilioni.

Jumla ya fedha zote zilizohamishwa ili “kuzitengenezea uhalali wa kuzichota,” zilikuwa Sh. 43.4 bilioni.

Mtandao huu umebaini kuwa nyaraka za uhamishaji fedha kutoka TPA kwenda BoT, zilipokewa saa 08.47, mchana wa Jumanne, tarehe 23 Machi 2021, na kufanyiwa uhamisho kwenda NMB kwa mafungu, kabla ya kurejeshwa kesho yake kwa maelekezo kutoka juu.

Mabilioni hayo ya shilingi BoT kutoka NMB, kutokana na kuvuja kwa taarifa za uhamishaji huo hadi kumfikia Rais Samia, ambaye aliagiza “kurejeshwa fedha hizo serikalini, mara moja.”

Nyaraka ambazo gazeti hili limeona zinaonyesha kuwa mkurugenzi huyo aliyesimamishwa kazi, aliidhinisha uhamishaji huo wa fedha, kwa kutumia dokezo lenye Kumb. Na. CD.199/600/01-B/66 la tarehe 22 Machi mwaka huu, lililotoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Evance Bahati.

Siku ambayo Mhandishi Kakoko aliidhinisha uhamishaji huo – tarehe 22 Machi – ilikuwa ni siku maalum ya mapumziko. Serikali ilitangaza siku hiyo, kuwa ni mahususi kwa wananchi na viongozi, jijini Dar es Salaam na viunga vyake, kupata nafasi ya kuaga mwili wa Dk. Magufuli.

Kwa mujibu wa dokezo hilo, fedha ziliidhinishwa kuhamishwa kwa kugawanywa katika mafungu manne:
• Akaunti ya matumizi ya kawaida Sh.13,707, 591, 625.52
• Akaunti ya matumizi ya kawaida dola za Marekani 80,464.47
• Akaunti ya matumizi ya maendeleo, Sh. 2,614,081,963.64
• Akaunti ya matumizi ya maendeleo inayotumia dola za Marekani, ni 11,718, 893.44

Akiandika kwa Meneja wa Banking Department, ndani ya Benki Kuu, mtaa wa Mirambo 1184, P.o Box 2939, Dar es Salaam, tarehe 23 Machi 2021, Kakoko aliekeza fedha hizo, ikiwamo Sh. 5.2 bilioni, kuhamishwa kutoka akaunti mbalimbali za shirika hilo.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Miongoni mwa akaunti hizo, ni akaunti ya makusanyo Na. 9925260081, yenye jina Tanzania Ports Authority and Collection Account, iliyoko BoT kwenda akaunti nyingine ya TPA iliyoko NMB, ambayo imebeba Na. 22310026141.

Taarifa zinasema, fedha zilihamishwa kwa ajili ya kulipia watoa huduma mbalimbali na watu wengine ambao hawakuweza kufahamika mara moja.

Dokezo lilisema, mabilioni hayo ya shilingi ni kwa ajili ya matumizi ya mwezi Machi 2021, awamu ya 17A (Phase 17A).

Hata hivyo, taarifa zinasema, matumizi yote ya TPA nchi nzima, kwa mwezi hayazidi Sh. 5 bilioni, ikiwemo Makao Makuu ya TPA, bandari ya Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Mwanza na Kigoma, jambo ambalo limeibua hisia kuwa fedha hizo zilikua zitumike nje ya matumizi ya lazima ya TPA.

Kuna madai ya utetezi kwamba sehemu ya fedha hizo zililenga kumlipa mkandarasi mmoja ambaye anafanya kazi mbalimbali za TPA, lakini zimeibua utata hasa kutokana na uharaka wa malipo yalivyofanyika, ikiwamo kipindi hichi cha maombolezo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Takukuru, Kamishna Hamduni amelenga kuifanya taasisi hiyo, kufanya kazi zake kwa weledi, ikiwamo kukamilisha uchunguzi wa kesi zote kubwa zilizopo ndani ya taasisi hiyo.

Kwa mujibu wa vyanzo vya taarifa, lengo la kukamilisha uchunguzi mapema, ni kuhakikisha Takukuru haizidiwi na mlundikano wa kesi na kutenda haki.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Kasilda Mgeni anasisitiza umoja, ushirikiano Same 

Spread the love  MKUU mpya wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda...

Habari MchanganyikoTangulizi

Hii hapa kauli ya Sheikh mpya mkoa wa Dar

Spread the loveSAA chache baada ya kuteuliwa kukaimu nafasi ya aliyekuwa Sheikh...

Habari MchanganyikoTangulizi

Breaking news! Mufti amng’oa Sheikh mkoa Dar

Spread the loveBARAZA la Ulamaa la Bakwata katika kikao kilichofanyika tarehe 1...

Habari Mchanganyiko

Bilioni 120 za DMDP zaibadilisha Ilala, wananchi watoa ya moyoni

Spread the loveJUMLA ya Sh bilioni 120.7 zimetumiwa na Halmshauri ya Jiji...

error: Content is protected !!