Monday , 29 May 2023
Home Gazeti Habari za Siasa NEC yapigwa stop na Mahakama kwa Nassari
Habari za SiasaTangulizi

NEC yapigwa stop na Mahakama kwa Nassari

Joshua Nassari
Spread the love

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dodoma, imetoa amri ya kuzuia kufanyika uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Arumeru Mashariki, hadi shauri la madai Na. 22/2019, lililofunguliwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Joshua Nassari, litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Mahakama Kuu mjini Dodoma, amri hiyo ya mahakama imetolewa kufuatia Nassari, kufungua shauri hilo mahakamani hapo.

Nassari amefungua shauri hilo tarehe 18 Machi 2019 na leo Jumatano ya tarehe 20 Machi, mahakama imeweza kutoa zuio. Shauri hilo limefunguliwa chini ya hati ya dharula.

Katika kesi hiyo, mbunge huyo wa Chadema anaomba mahakama kutoa ruhusa ya kumshitaki Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ili kufungua shauri la kufuta; na kutengua uamuzi wa Spika wa Bunge wa kumvua ubunge.

Kesi iliyofunguliwa na Nassari dhidi ya Spika Ndugai na mwanasheria mkuu wa serikali, iko mbele ya Jaji L. Mansoor.

“…baada ya Mahakama Kuu kanda ya Dodoma, kusikiliza pande zote mbili zinazohusika katika shauri hilo, Jaji Mansoor ameutaka upande wa majibu maombi, kuwasilisha majibu ya madai ya Nassari, kisha tarehe 27 Machi mwaka huu, shauri litaanza kusikilizwa,” ameeleza mmoja wa wanasheria wa Nassari aliyezungumza na gazeti hili.

Kwenye hati yake ya kiapo, Nassari amekana madai ya Spika Ndugai kuwa hajahudhuria vikao vya Mikutano Mitatu mfululizo ya Bunge na amelalamika “kuhukumiwa na Spika Ndugai bila kusikilizwa.”

Taarifa za ndani ya Bunge zinasema, Nassari alihudhuria vikao vya Kamati za Bunge kwenye mkutano wa Novemba mwaka jana na alisaini fomu ya mahudhurio na alilipwa stahiki zake.

Nassari, ni mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

Aidha, Nassari ameeleza katika malalamiko yake kuwa alimjulisha Spika Ndugai sababu za kushindwa kuhudhuria mkutano uliyopita kwa barua; alichukua hatua hiyo kabla ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge wa Januari.

Joshua Samweli Nassari, alitangazwa kuvuliwa ubunge na Spika Ndugai, tarehe 14 Machi mwaka huu, kufuatia madai ya kushindwa kuhudhuria “vikao vya Mikutano Mitatu mfululizo ya Bunge.”

Mikutano hiyo ilitajwa na Spika, ni mkutano wa 12 wa tarehe 4 hadi 14 Septemba 2018, mkutano wa 13 wa tarehe 6 hadi 16 Novemba 2018 na mkutano wa 14 wa tarehe 29 Januari hadi 9 Februari mwaka huu.

Taarifa ya Bunge ilieleza pia kuwa tayari Spika Ndugai amemwandikia  barua Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistacle Kaijage, kumtaarifu kuwa jimbo la Arumeru Mashariki lipo wazi, kutokana na mbunge wake kupoteza sifa za kuendelea kuwa mbunge.

“Tume ya taifa ya uchaguzi inaweza kuendelea na mchakato wa kumpata mbunge wa kujaza nafasi hiyo iliyo wazi ya jimbo la Arumeru Mashariki,” ilieleza sehemu ya taarifa ya Bunge ya kutangaza maamuzi ya Spika Ndugai ya kumvua ubunge Nassari.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Uamuzi juu ya wakurugenzi kusimamia uchaguzi 13 Juni

Spread the love  MAHAKAMA ya Afrika ya Haki za Binadamu (ACHPR), imepanga...

Habari MchanganyikoTangulizi

Jeshi la Polisi kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika utafiti

Spread the love  JESHI la Polisi Nchini limesema kuwa katika kukabiliana na...

KimataifaTangulizi

Mtuhumiwa wa mauaji ya halaiki ya Rwanda akamatwa Afrika Kusini

Spread the love  MMOJA wa watuhumiwa wakuu wa mauaji ya Kimbari ya...

Habari za Siasa

Musoma Vijijini waomba ujenzi wa barabara uanze haraka

Spread the loveJIMBO la Musoma Vijijini, mkoani Mara, limeomba Serikali kuhakikisha ujenzi...

error: Content is protected !!