July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waliokimbia vita Syria, wafia msikitini New Zealand

Spread the love

HAMZA Mustafa (15) na baba yake aliyetajwa kwa jina moja Khalid (44), raia wa Syria waliokimbilia New Zealand, waliuawa kwenye mashambulizi yaliyotokea msikitini nchini humo siku tano zilizopita. Inaripoti mitandao ya kimataifa … (endelea).

Miongoni mwa majina ya waliouawa kwenye mashambulizi hayo yaliyotokea kwenye msikiti wa Al Noor na Lin Wood ni Hamza na baba yake Khalid.

Wawili hao walipoteza maisha huku kijana mdogo wa marehemu Khalid, Zaed akijeruhiwa kwa risasi katika tukio hilo, ikiwa ni miezi sita kupita tangu walipoingia nchini New Zealand wakitokea Syria.

Tayari baadhi ya miili  ya watu waliopoteza maisha katika shambulio hilo katika mji wa Christchurch, New Zealand imetambuliwa na kukabidhiwa kwa familia zao kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Jacinda Arden, Waziri Mkuu wa New Zealand amesema, takribani miili 30 imetambuliwa na kukabidhiwa kwa familia zao kwa ajili ya kuzikwa.

Miili mingine iliyozikwa leo Jumatano tarehe 20 Machi 2019 ni pamoja na mwili wa Junaid Ismail (36) na Ashraf Ali (58).

Imam wa Kituo cha Kiislamu nchini Australia aliyefika nchini New Zealand kwa ajili ya kushiriki shughuli za mazishi, Mohamed Aljibaly alisema, taarifa zinaonesha kuwa raia hao wa Syria waliofariki dunia katika tukio hilo, waliikimbia nchi yao na kuwasili New Zealand wakiamini kwamba, ni sehemu salama ya kuishi lakini walipoteza maisha kwa kupigwa risasi.

Tukio hilo  lilitokea Ijumaa ya tarehe 15 Machi 2019 alfajiri katika misikiti ya Al Noor na Lin Wood. Watu takribani 50 walipoteza maisha wakati 48 wakijeruhiwa.

Majeruhi 29 katika tukio hilo wanatibiwa katika hospitali ya Christchurch, huku wanane kati yao wakiwa katika hali mbaya.

Miongoni mwa watu walio mahtuti ni pamoja na mtoto wa kike wa miaka minne anayepatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Starship iliyoko maeneo ya Auckland mjini Christchurch.

error: Content is protected !!