March 8, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kuelekea 2020: Ndugai aanza kumpigia chapuo Rais Magufuli

Rais John Magufuli (kulia) akiteta jambo na Spika wa Bunge, Job Ndugai

Spread the love

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, ameanza kampeni ya kumnadi Rais John Magufuli. Ameagiza kuandaliwa muswada wa Bima ya Afya kwa wote, kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Akizungumza bungeni, Spika Ndugai alisema, “ninaeleekeza serikali, kufanya kazi usiku na mchana, ili kuandaa muswada wa Bima ya Afya kwa wote. Ninataka muswada huu, uletwe hapa bungeni na kupitishwa kabla ya mwaka 2020.” 

Spika Ndugai alitoa kauli hiyo, leo asubuhi, tarehe 4 Februari 2019, wakati wa kipindi cha maswali na majibu.

Alisema, serikali inapaswa kutoa Bima ya Afya kwa wananchi wake wote ili iwe zawadi kubwa kwa Rais Magufuli kwa wananchi wake kabla ya kufika uchaguzi mkuu ujao.

“…Wenzetu serikalini, kabla ya uchaguzi mwakani, kuwe na uwezekano wa kupatikana huduma ya afya kwa wote. Nawaomba mfanye kazi usiku na mchana kufanikisha jambo hili. Hii itakuwa zawadi kubwa kwa rais kwa wananchi wake,” ameeleza Spika Ndugai.

Aliongeza: “Tunawaomba sana jambo hili lipate msukumo wa kipekee, ili Watanzania wapate mfuko wa Bima ya Afya kwa wote.”

Kauli ya Spika Ndugai imekuja muda mfupi baada ya  Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, kuliambia Bunge kuwa “serikali iko katika mwelekeo wa kwenda kwenye mfumo wa bima moja ya afya kwa wananchi wote.”

Dk. Ndugulile amewaomba wabunge kuunga mkono muswada huo pindi utakapowasilishwa bungeni. Dk. Ndungulie alikuwa akijibu swali la msingi la mbunge wa Viti Maalum (CCM), Kiteto Koshuma.

Oktoba mwaka juzi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluhu Hassan alisema, ili kumpunguzia mzigo wa gharama za matibabu mwananchi wa kawaida, serikali imeandaa muswada wa Bima ya Afya kwa wote utakaowezesha kila mwananchi kuwa na uhakika wa matibabu.

Alitoa kauli hiyo wakati akizindua kongamano la 49 la afya jijini Dar es Salaam.

error: Content is protected !!