April 11, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kosa la Mbatia ni lipi?

Spread the love
MIJADALA kwenye mitandao ya kijamii, imekoleza tuhumadhidi ya Mwenyekiti wa taifa wa chama cha NCCR- Mageuzi, James Francis Mbatia, kwamba anatumika na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kudhoofisha upinzani. Anaandika Yusuph Katmba, Dar es Salaam … (endelea). 

Kisa: Ni hatua ya Mbatia, kusafiri hadi mkoani Mbeya, kujenga chama chake.  

Mbatia yuko mkoani humo kwa ziara ya siku 7 ambapo, pamoja na mambo mengine, anatarajiwa kufungua ofisi mpya ya NCCR- Mageuzi, jijini Mbeya.

Yote haya yanalenga kujipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao wa rais, wabunge na madiwani. Uchaguzi mkuu wa rais, unatarajiwa kufanyika 25 Oktoba mwaka huu.

Katika ziara hiyo inayotajwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa yenye manufaa makubwa, Mbatia amepokea mamia ya wanachama wapya wa chama chake. 

Miongoni mwao, ni waliokuwa viongozi wandamizi wa Chadema, katika jimbo la Busekelo, Furaha Mwakalundwa, ambaye alikuwa mwenyekiti na Anyabwile Mwansile, aliyekuwa katibu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Busekelo, uongozi wote wa Chadema katika jimbo hilo, ikiwamo kamati tendaji, imejiuzulu na kujiunga na NCCR- Mageuzi.

Kuanza kung’ara upya kwa nyota ya NCCR- Mageuzi mkoani Mbeya, kumetokana na kazi inayofanywa na Boniface Mwabukusi, aliyetangaza kujitenga na Chadema wiki mbili zilizopita na kujiunga na chama cha Mbatia. 

Baadhi ya wanaomtuhumu Mbatia kutumika, wanadai kuwa ni kosa kwa mwanasiasa huyo kupokea watu waliokuwa wanachama wa Chadema. Kwamba, kwa kufanya hivyo, Mbatia anatumika kudhoofisha chama hicho na upinzani kwa jumla wake.

Aidha, wanaomtuhumu Mbatia wanadai kuwa hatua yake ya kwenda kukutana na Rais John Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam na baadaye kumtembelea mkuu wa mkoa wa Mbeya, ofisini kwake, kunathibitisha madai kuwa mwanasiasa huyo anatumika. Mimi nitajadili yote mawili:

Kwanza, siyo kosa hata kidogo Mbatia kukutana na Rais Magufuli na kujadiliana naye mambo mbalimbali; na au kutembelea ofisi ya mkuu wa mkoa. Hili siyo kosa.

Mbatia ni kiongozi wa kitaifa wa moja ya vyama vya siasa mashuhuri nchini – NCCR- Mageuzi. Ni mbunge. Na kwa sasa, ni mwenyekiti wa taasisi jumuishi ya vyama vya siasa, iitwayo Tanzania Center for Democracy (TCD). 

Mbatia anajua kuwa moja ya sera kuu ya chama anachokiongoza – kabla na baada ya kurejea tena kwa mfumo wa vyama vingi nchini – ni “kupingana bila kupigana.” Hili analijua; naye amekuwa akiishia kwa matendo hayo. 

Boniphace Mwabukusi, mwanachama mpya wa NCCR-Mageuzi

Katika semina iliyofanyika katika chuo cha CCM, Kivukoni, jijini Dar es Salaam, mwanzoni mwa Oktoba 1991, wajumbe wa Kamati ya Katiba na Mageuzi, walieleza msimamo wao bayana mbele ya mwenyekiti, makamu mwenyekiti na katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, kwamba “Tanzania inahitaji amani.”

Lakini wajumbe walieleza, “kuwapo au kudumu kwa amani, kusiwe na maana kwamba wananchi waache upinzani dhidi ya udikteta wa chama kilichoko madarakani.” 

Kwamba, malengo ambayo waliyapigania yeye Mbatia na wenzake – Mabere Nyaucho Marando, Christopher Kasanga Tumbo, Prince Mahinja Bagenda, Omar Aweis Dadi, Dk. Ringo Tenga, Shaban Hamis Mloo, Ndimara Tegambwage, Anthony Komu na wengineo – sasa hayapo tena.

Kwamba, taifa lililokuwa likisifika kwa ukuaji wa utawala bora na uhuru wa kujieleza, kila pembe ya nchi linatuhumiwa kukandamiza haki za raia wake. Taifa lililokuwa mstari wa mbele kudai haki za wengine, kila uchao sasa, wananchi wake wanalalamika, nchi yao kurejeshwa nyuma miaka kenda katika eneo hilo.

Hivyo basi, kwa vyovyote vile, Mbatia hakupaswa kutokwenda Ikulu. Alipaswa kwenda ili kumueleza bayana rais kuwa kinachotendeka sasa, siyo kile ambacho walikipigania. Amefanya hivyo.

Kutenda tofauti na hivyo, ni kutojitendea haki yeye mwenyewe, chama chake na wananchi kwa ujumla.

Kuhusu madai kuwa Mbatia ametenda “jinai ya kisiasa,” kutokana na uamuzi wake wa kukutana na mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila; tuhuma hiyo, nayo haina mashiko.

Sote tunajua kuwa jukumu kuu la ulinzi wa raia na mali zao, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri, limekabidhiwa kwa serikali. Hatua ya Mbatia kufika ofisini kwa mkuu wa mkoa, ililenga siyo tu kujenga mahusiano mema, kati yake binafsi na mkuu wa mkoa, bali pia kuondoa hofu ya kibinadamu kwa kila mmoja.

Pili, wapinzani wa Mbatia, wanabeza kubeba wanachama wa Chadema na kuwapa kadi za NCCR- Mageuzi. Wanasema, “huu ni mradi maalum unaoratibiwa na chama tawala ili kudhoofisha chama chao.” Hii ni hoja mfu.

Hakuna kokote ambako kumetajwa kuwa ni kosa, kwa mwanachama ama kiongozi wa chama kimoja cha siasa, kujiunga na chama kingine. Hakuna. 

Kwa takribani miaka 10 sasa, viongozi mbalimbali wa vyama vya NCCR- Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF) na pengine Tanzania Lebour Party (TLP), wamekuwa wakivihama vyao na kujiunga na Chadema.

Kwa mfano, kabla ya kujiunga na Chadema, Willifred Muganyizi Lwakatare, mbunge wa sasa wa Bukoba Mjini, alikuwa kada mahiri wa CUF. Ndani ya chama hicho, Lwakatare alifikia kushika wadhifa wa naibu katibu mkuu (Bara). 

Aliondoka CUF mwishoni mwa mwaka 2010. Lakini CUF ambayo wakati huo, kilikuwa bado kiko imara, haikuwahi kulalamikia Chadema kutumika, kukidhoofisha.

Naye Prof. Mwesiga Baregu, Mabere Marando, Joseph Selasini, Tundu Lissu, Anthony Komu na wengineo, kabla ya kujiunga na Chadema, walikuwa wanachama wandamizi ndani ya NCCR- Mageuzi. 

Marando alikuwa mwenyekiti wa kwanza mwanzishi wa chama hicho; mwasisi aliyekuwa akimiliki kadi Na. 1 na katibu mkuu wa pili. Baregu alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu na mshauri mkuu wa mwenyekiti.  

Naye Komu, mbunge wa Chadema katika jimbo la Moshi Vijijini,  ndani ya NCCR- Mageuzi, alihudumu kwenye nafasi ya naibu mkurugenzi mtendaji. 

Selasini, mbunge wa sasa wa Rombo, mkoani Kilimanjaro, akitajwa kushika nafasi ya mkurugenzi wa habari na uenezi.

Lakini pamoja na wote hao kujiunga na Chadema, Mbatia na NCCR- Mageuzi yake, haikulalamika. Haikutuhumu Chadema kuwadhoofisha. Haikutukana. 

Badala yake, walijitafakari na kujitathimini. Wakachukua kioo na kujiangalia wapi walikoteleza. Kipi kimewasukuma waasisi wake, kukimbia chama chao. 

Kazi hii takatifu, ndiyo iliyopaswa kufanywa na Chadema. Siyo kugombana na kushambulia chama kingine au kutukana wanaokihama.

Hii ni kwa sababu, wengi wanaohama Chadema, ni wale waliochoshwa na kile wanachoita, “kilevi cha mafanikio ya  ukuaji wa chama chao, kilichowalevya baadhi ya viongozi wake.” Sababu nyingine inayotajwa, ni “magomvi ya ndani kwa ndani na ubaguzi.” 

Kwa muktadha huo, Chadema hakipaswi kulaumu NCCR- Mageuzi. Hakipaswi wanachama wake au viongozi kutukana. Kinapaswa kukaa chini na kujitafakari, ili kisiruhusu kutumbukia kule walikokwenda wengine. Ni kwa sababu, kujenga ni ngumu, lakini kubomoa, ni rahisi.

error: Content is protected !!