May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kigogo MSD aelezea alivyosota rumande miezi 11

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu

Spread the love

 

LAUREAN Bwanakunu, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa nchini (MSD), amesema Hayati Padri Privatus Karugendo ni miongoni mwa watu waliomtia moyo wakati akiwa rumande katika Gereza la Segerea, jijini Dar es Salaam. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam…(endelea).

Bwanakunu ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, tarehe 28 Juni 2021, katika ibada ya kuuaga mwili wa Padri Privatus, iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Roho Mtakatifu Segerea, jijini Dar es Salaam.

Padri Privatus alifariki dunia usiku wa kuamkia tarehe 24 Juni 2021, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na mwili wake umezikwa leo katika makaburi ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam.

Akizungumza katika ibada hiyo, Bwanakunu amesema alipokuwa mahabusu katika gereza hilo katika kipindi cha miezi 11 (Juni 2020-Mei 2021), Padri Privatus alikuwa anampelekea vitabu vilivyobeba ujumbe wa kumtia moyo na kumpa matumaini.

“….Aprili 2020 niliondolewa kazi niliyokuwa nafanya, miezi mmoja baadaye nikapelekwa mahabusu ilikuwa ni mwezi wa sita mwaka jana, nilikaa miezi 11. Baada ya hapo Father Privatus akaja kunitembelea gerezani.

“Akaniletea vitabu vingi sana mpaka mkuu wa gereza akasema mbona vingi mmeficha nini humo ndani? lakini akajieleza akafanikiwa kuviingiza, akanipa maneno ya kunitia faraja,” amesema Bwanakunu.

Kigogo huyo wa zamani wa MSD amesema, Padri Privatus hakumuacha, hata alipotolewa mahabusu aliendelea kuwa karibu nae na kwamba kabla ya mauti kumfika, waliweka miadi ya kuonana.

“Nilivyotoka mahabusu gerezani mwezi mmoja uliopita, nilikaa bila kwenda mahakamni akanipigia simu akanipa pole. Nikamwambia nimetoka naenda kijijini kwetu kufanya ibada, nilikuwa nimeshaenda tayari akaniambia mbona hukuniambia ningekusindikiza tufanye wote ibada.  Huyo ndio Father Privatus. Na kweli alikuja,” amesema Bwanakunu.

Bwanakunu ameongeza “nilivyorudi na sasa juzi kama tarehe 12 Juni 2021, akaniandikia ujumbe ambao sasa ni ujumbe wake kwangu wa mwisho akasema hivi omwana wa tata tutafurahi sana kujua ratiba yako ukirudi Dar es Salaam, tungependa kuja kukuona ila tunajua Covid-19 tusingependa sogeza msongamano, wengi wanataka kukuona. Tuandalie ratiba siku nzuri ya kukuona.”

Bwanakunu na aliyekuwa Mkurugenzi wa Logistiki MSD, Byekwaso Tabura, waliachwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu tarehe 13 Mei 2021, baada ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtakata nchini (DPP), Biswalo Mganga, kutoonesha nia ya kuendelea na kesi ya uhujumu uchumi, iliyokuwa inawakabili.

Kwa mara ya kwanza Bwanakunu na Tabura walifikishwa kizimbani tarehe 5 Juni 2020, wakikabiliwa na mashtana matano ikiwemo utakatishaji fedha zaidi ya Sh. 1.6 bilioni.

Shtaka lingine ni kuisababishia hasara MSD ya Sh. 3.8 bilioni, kosa wanalodaiwa kufanya kati ya Julai 1 2016 na Juni 20, 2019.

error: Content is protected !!