Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kutokana na uchakavu wa vivuko vya sasa vinavyotoa huduma kati ya Kigamboni na Kivukoni (Ferry), Serikali imepanga kununua kivuko kipya chenye uwezo wa kubeba abiria wengi na mizigo mingi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 6 Disemba, 2021 aliposimama kuzungumza na wananchi wa Kigamboni akiwa anaelekea katika uzinduzi wa Kiwanda cha Elsewedy Electric East Africa Ltd cha utengenezaji wa nyaya za umeme na transfoma.

Aidha, akizungumzia kero zilizowasilisha na Mbunge wa Jimbo hilo, Dk. Faustine Ndugulile (CCM), Rais Samia amesema katika suala la tozo magari zinazotozwa katika daraja la Nyerere ameahidi kulifanyika kazi.

“Nataka nilichukue, niwaahidi nitakwenda kulifanyia kazi, nitakwenda kukaa na taasisi husika ili niliwasilishe kama alivyowasilisha ili lifanyiwe kazi.

“Suala la barabara, naomba niachie… nawe jikaze kule bungeni tutakapowaletea bajeti ya mwakani sema kwa sauti kubwa, nami nitalibeba nitalishughulikia, ” amesema.

Ameongeza kuwa Kigamboni ni eneo jipya lakini ni dhahiri kwamba mkoa wa Dar es Salaam ni mji wa zamani lakini haukuwa na barabara za lami mitaani.

Amesema maeneo mengi yameanza kupata barabara za lami miaka mitano, sita iliyopita hivyo si ajabu kuona Kigamboni haina barabara nyingi za lami.

“Nimetoka Mbagala juzi tatizo ni hilihili, lakini yote ni maeneo mapya kwa hiyo lengo letu Dar es Salaam mkoa mzima uwe na barabara za lami kwa sababu ndio lango la Tanzania ndio jiji la biashara, na wawekezaji wanaelekea maeneo mbalimbali.

“Wako Pwani, Mkuranga wako maeneo mengine na Kigambon tunaanza kuifungua kwa viwanda kwa hiyo lazima tuwe na barabara za lami, naomba mniachie nikayafanyia kazi na jawabu mtalisikia kuanzia bajeti ya mwaka,” amesema.

Awali Dk. Ndugulile alimkumbushia Rais kwamba tarehe 8 Septemba, 2020 alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa kampeni za mgombea ubunge Kigamboni ambapo pamoja na mambo mengine, aligusia suala la barabara.

“Katika barabara za Tanroad Kigamboni, asilimia 37 tu zimepigwa lami na katika asilimia 100 za barabara ambazo hazijapigwa lami katika mkoa wa Dar, asilimia 50 ziko Kigamboni.

“Pia kuna barabara za ndani, Kigamboni ni mji ambao umepangwa, asilimia zaidi ya 70 tumeupima, barabara zipo lakini ukiangalia katika mioundombinu ya TARURA kuna zaidi ya kilomita 1,000 lakini zilizopigwa lami ni kilomita tano sawa na asilimia 0.5. Kwa hiyo kipaumbele changu cha kwanza na kilio cha wana-Kigamboni ni barabara, cha pili ni barabara,” amesema.

Kuhusu daraja la Nyerere, Dk. Ndugulile amesema licha ya wananchi wa Kigamboni kushukuru kwa ujenzi wa daraja hilo ambalo ni ukombozi mkubwa lakini kuna changamoto kuhusu tozo.

“Sisi Kigamboni hatuna ruti ndefu, kama za wenzetu, tunahitaji ruti tatu, nne kufika mjini, lakini daladala moja ikivuka daraja la Nyerere, ruti moja inatozwa Sh 5,000, ikipiga tripu 10 kwenda na kurudi ni Sh 100,000 anaiacha darajani… hapo hajaweka hela ya mafuta, tajiri na hela yake.

“Kwa hiyo wananchi wa Kigamboni wanakuomba sana tuende tukaliangalie jambo hili, jinsi gani tunaweza kuleta nafuu kwa wananchi wa Kigamboni na kufanya maiosha yao yawe mepesi,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *