RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemwapisha Profesa Adelardus Kilangi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Profesa Kilangi, ameapishwa leo Jumatatu, tarehe 6 Desemba 2021, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Anakwenda kuchukua nafasi ya Emmanuel Nchimbi ambaye alihudumu nafasi hiyo kuanzia Februari 2017, baada ya kuteuliwa na aliyekuwa Rais wa wakati huo, Hayati John Pombe Magufuli.
Haijafahamika, kama Nchimbi ambaye amewahi pia kuwa waziri wa mambo ya ndani katika utawala wa awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, anarejea nchini au amepangiwa kituo kingine cha kazi.
Kabla ya kuteuliwa kwa Profesa Kilangi kuwa Balozi, tarehe 12 Septemba 2021, alikuwa mwanasheria mkuu wa serikali (AG).
Nafasi hiyo ya mwanasheria mkuu wa serikali, aliteuliwa Dk. Eliezer Feleshi, ambaye alikuwa Jaji Kiongozi wa Tanzania.
Profesa Kilangi, aliteuliwa kuwa mwanasheria mkuu wa serikali, tarehe 1 Februari 2018, akichukua nafasi ya George Masaju, aliyeteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.
Leave a comment