October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya Mbowe: Shahidi asimulia alivyoteswa akiwa amevuliwa nguo zote

Spread the love

 

ADAM Kasekwa, mshtakiwa wa pili katika kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi amieleza Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kuwa baada ya kukamatwa, alivuliwa nguo zote kisha akateswa akiwa amening’inizwa kwenye kichuma mithiri ya popo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Kasekwa ni miongoni mwa mashahidi katika kesi ndogo ndani ya kesi kubwa inayowakabili yeye pamoja na wenzake akiwemo kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe.

Mbali na Mbowe na Kasekwa wengine; ni Halfan Bwire Hassan na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Kasekwa ambaye ni mshtakiwa kwenye kesi hiyo, ameanza kutoa utetezi wake leo Ijumaa, tarehe 24 Septemba 2021, baada ya upande wa Jamhuri kufunga utetezi wao.

Jamhuri iliyopanga kutumia mashahidi saba, imeieleza mahakama hiyo kwamba inawaondoa mashahidi wanne iliyotaka kuwatumia.

Tayari mashahidi watatu walikwisha kutoa ushahidi wao ambao ni Kamanda wa Polisi wa Kinondoni (RPC), Ramadhan Kingai, Inspekta Mahita Omari Mahita na Askari Polisi, Ricado Msemwa.

Kabla ya Kasekwa kuanza kujitetea, wakili wake John Mallya amesema, watakuwa na mashahidi wanne akiwemo Kasekwa mwenyewe.

Akiongozwa na Mallya kutoa ushahidi, aliulizwa alikuwa nani amedai alikuwa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kikosi namba 92 Sangasanga mkoani Morogoro.

Alipoulizwa ni kikosi cha namna gani amejibu akisema ni kikosi cha makomandoo lakini sasa kinaitwa ‘special force.’

Akijibu swali aliloulizwa kwamba amehudumu jeshini kwa kipindi gani amesema miaka sita kati ya mwaka 2012 hadi 2018.

Amedai, mwaka 2016 hadi 2017 alikuwa misheni nchini Congo na alilerea salama na kuendelea na kazi.

Mallya alimuuliza ilikuwaje akaacha kazi, Kasekwa amedai, hakuacha kazi bali aliachishwa kazi na wakuu wake baada ya kugundua alikuwa na tatizo la Battle Confusion.

Alipoulizwa ni tatizo gani hasa hilo, amedai hawezi kulijua zaidi lakini ni hali ya askari anaposikia milio ya mizinga na risasi kwa wingi anakuwa hafanyi vile anavyotakiwa na wakubwa zake.

Amedai, kabla ya kuachishwa kazi alipata matibabu katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugola, Dar es Salaam.

Akijibu swali la Wakili John Mallya kwamba baada ya kuachishwa kazi, alikuwa anajishughulisha na nini, mshtakiwa huyo amedai alikuwa anafanya biashara ya kununua maharage huko Morogoro sehemu inaitwa Nongwe na kuuza soko la Lubeho mkoani humo.

Kasekwa alipoulizwa, anakumbuka nini tarehe 5 Agosti 2021, ameieleza mahakama akiwa na mshitakiwa mwenzakenamba tatu, Mohammed Ling’wenya, sehemu inaitwa maduka, Moshi mkoani Kilimanjaro, walivamiwa na watu kama watano.

Amedai, walimvamia yeye kwanza na kuanza kumpiga na mshatakiwa mwenzake akafika ili kumsaidia.

Ameendelea kudai, alipofika Ling’wenya aliuliza kwa nini wanampiga na yeye akaulizwa kama ananifahamu akawajibu ndio.

Kasekwa amedai, wakati akiendelea kupigwa, akasikia hao waliokuwa wanampiga wakisema ana madawa na silaha.

Alipoulizwa kama watu hao waliohusika kumkamata na kumpiga anawakumbuka, Kasekwa ameielea mahakama anawakumbuka ni Ramadhani Kingai na Mahita ambao amewafahamu majina yao hapo mahakamani kwani muda mwingi wa matukio walikuwepo.

Akijibu swali aliloulizwa na Wakili Mallya kwamba watu hao wawili amewataja walikuwa na majukumu gani, Kasekwa amejibu akidai, amewatambua kwa kuwa sura na matendo yote ya kumpiga na kumwekea madawa na silaha walikuwapo.

Jaji Mustapha Siyani anayesikiza kesi hiyo, akamuuliza Kasekwa, anaposema kumwekea madawa na silaha nini kilitokea.

Akijibu swali hilo, Kasekwa amedai wakati anapigwa na kubanwa, waliingiza mkono kwenye suruali yake akasema ana madawa na mwingine akaingiza kitu nyuma ya mkanda akatoa kitu akasema ni silaha.

Amedai baada ya kumtoa pale walipomkamatia, walimpeleka kituo cha polisi ambacho amekuja kukijua jina lake kuwa ni Central Moshi hapo mahakamani.

Alipoulizwa baada ya kufikishwa hapo nini kilifuata, Kasekwa amedai walimfikishia kwenye chumba kisha baadaye walimtoa na kumpeleka kwenye chumba cha pembeni palipokuwana jopo la watu wengi ambapo walimvua nguo akawa ananing’inia kwenye kichuma mithiri ya mshikaki au popo.

Amedai, baada ya mateso hayo aliyoyapata Moshi, alisafirishwa hadi Tazara jijini Dar es Salaam akiwa amefunikwa usoni tarehe 7 Agosti. Ilipofika tarehe 9 Agosti, walimtoa Tazara usiku ambapo anadai alikuwa ana uwezo wa kutembea huku akielezwa anakopelekwa anakwenda kukutana na kilichomtokea Moshi.

Kasekwa amedai, safari hiyo haikuwa ndefu kama ya kutoka Moshi hadi Dar es Salaam, ilikuwa fupi ingawa alikuwa amefunikwa usoni kwa jaketi haoni kinachoendelea.

Wakiwa wamefika Mbweni, Kingai aliyekuwepo na akamtaja mtu mwingine anaitwa Goodluck wakamweleza, kadri mateso yanapopungua, kuna mambo mazuri yanakuja na kumweleza pia, kuna nyaraka wanampelekea wanamtaka azisaini.

Kasekwa amedai, alipofikishwa kituoni hapo, alipewa kikaratasi akaelezwa atakuwa anaitwa Vicent Juma na akiulizwa amekamatiwa wapi ajibu Tabora kwa kesi ya ungang’anyi.

Amedai walimpeleka nyaraka hizo na kuzisaini bila kujua zinahusu nini.

Mshtakiwa huyo ameionesha mahakama maeneo aliyoteswa na kuumizwa ambayo ni mkononi na mguuni na kudai, kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja tangu apate mateso hayo, hakuwahi kupelekwa hospitalini.

Ameieleza mahakama hiyo kuwa alikaa kituoni hapo Mbweni hadi alipofikishwa mahakamani tarehe 19 Agosti 2020 na wakati wote hawawahi kufunguliwa pingu.

Kesi inaendelea…

error: Content is protected !!