Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kesi ya Mbowe: Mvutano waibuka kuhusu shahidi, Jaji aiahirisha
Habari za SiasaTangulizi

Kesi ya Mbowe: Mvutano waibuka kuhusu shahidi, Jaji aiahirisha

Spread the love

 

MVUTANO umeibuka baina ya mawakili wa utetezi katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu na ule wa Jamhuri. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Umeibuka wakati tayari shahidi wa sita wa Jamhuri, askari polisi SSP Sebastian Madembwe (46), ambaye ni Mrajisi wa leseni za bunduki wa Jeshi la Polisi akiendelea kutoa ushahidi wake, akiongozwa na Wakili wa Serikali, Pius Hilla.

Ni leo Alhamis tarehe 4 Novemba 2021, mbele ya Jaji Joackim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, iliyopo Mawasiliano jijini Dar es Salaam.

Mbali na Mbowe kwenye kesi hiyo, wengine ambao walikuwa makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Hassan Bwire, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Aliyeibua mvutano huo ni Wakili wa Utetezi, Jeremiah Mtobesya ambaye ameingia mahakamani kwa kuchelewa na mara baada ya kuingia, wakili anayeongoza jopo la utetezi, Peter Kibatala kumtambulisha, ndipo akaibuka hoja iliyoibua mabishano ya kisheria.

Fuatilia hapa ilivyokuwa;

Kibatala: Samahani Mheshimiwa Jaji. Naomba kwanza kumwombea Wakili Jeremiah Mtobesya aweze kuingia kwenye orodha yetu, ambaye amechelewa kwa sababu nilizotoa mwanzoni. Baada ya hayo nitaomba sasa wakili Mtobesya aweze kusema alichotaka.

Mtobesya: Mheshimiwa Jaji, shahidi hana maelezo katika kifurushi cha committal.

Mtobesya: Kwa hiyo ushahidi wake hauwezi kuingia kwa mujibu wa kifungu cha 246 cha CPA. Hakuna maelezo yake, na nimeulizana na wenzangu kama upande wa mashitaka uliomba mwanzoni ombi lolote. Nimeambiwa hapana.

(Mahakama inakaa kimya).

Mtobesya: Mheshimiwa Jaji, tutaomba pia maelekezo endapo wenzetu watafanya kwa usahihi, vipi kuhusu ushahidi ambao shahidi ameshaanza kuutoa hapa mahakamani.

Mtobesya: Na ninataatifiwa hapa na kaka yangu kwamba shahidi anatakiwa aondoke na ushahidi wake tuendelee na ushahidi mwingine kwa sababu hawawezi kupata faida baada ya sisi kusema kama wao hawakuomba mwanzoni.

(Mawakili wa Serikali wananong’onezana jambo).

(Jaji naye ameinama anaandika kidogo).

Wakili wa Serikali: Mheshimiwa Jaji, ombi hilo halina mashiko yoyote ya kisheria.

Jaji: Maombi au pingamizi?

Wakili wa Serikali: Ahaaa! Pingamizi halina mashiko yoyote ya kisheria kwa sababu limeletwa katikati ya ushahidi wa PW6 kinyume na sheria. Na kama wangekuwa na hoja hiyo walitakiwa kufuatilia mapema. Lakini kwa wakili ambaye hakufuatilia tangu mapema proceedings hizi … Hoja yetu ya pili ni kwamba shahidi huyu aliorodheshwa tangu kipindi cha commital proceedings na anasomeka kama shahidi namba 23 tangu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Na hata katika barua yetu ya 11 Agosti 2021.

Jaji: Ukurasa wa ngapi?

Wakili wa Serikali: Ukurasa wa 32 na jina lake linaonekana namba 23.

Wakili wa Serikali: Labda lile neno S liondoke isomeke Sebastian. Lakini substance ilikuwa committed na ilisomwa katika mwenendo wa shauri hilo katika proceedings za tarehe 23 mwezi wa nane siku ambazo commital proceedings zilifanyika. Na jina lake limeandikwa Sebastian Madembwe SSP.

Wakili wa Serikali: Lakini pia katika ile list ya exhibit katika ukurasa wa 33 nyaraka inayokuja kuzungumzia imekuwa listed pale namba 18 ambayo pia imesainiwa na Sebastian Madembwe SSP nilikuwa committed na substance yake ilisomwa. Kwa hiyo kwa namna yoyote ile hatukutakiwa kuleta ombi kupitia kifungu cha 289 cha CPA ili shahidi huyu aweze kutoa ushahidi wake.

Wakili wa Serikali: Na tunasema pia matakwa ya Rule 8 Sub 2 ya The Economic and Organized Crime (Corruption and Procedure Rules ya 2016) takwa hili la kisheria lilitekelezwa na Mahakama. Iwe jina ama substance ya ushahidi anaotoa leo hii hakuna kitu kipya kama ambavyo wakili anajaribu kuonyesha Mahakama yako tukufu.

Wakili wa Serikali: Na kama hali iko hivyo hakuna haja ya kutoa amri yoyote ile kutokana na ushahidi ambao umetolewa na shahidi kwa sababu shahidi yupo sahihi kwa mujibu wa sheria. Hivyo Mheshimiwa Jaji tunaomba hilo pingamizi ulitupilie mbali ili shahidi wetu aweze kuendelea na ushahidi wake.

(Jaji anaandika kidogo).

Mtobesya: Kwanza kabisa wenzangu wameni- attack personally. Sikuwapo kwenye proceedings tangu mwanzo. Mimi kuchelewa kufika sidhani kunaweza kuathiri. Sisi tunachofanya hapa ni kuisaidia Mahakama kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria. Nimesema kwenye commital documents hakuna ushahidi wa shahidi huyu.

Mtobesya: Substance inaongelea mambo matatu. Kwanza ni majina, ingawa yamekosea hatuna shida na hilo, pili cheti atakachotoa na tatu hakuna kile ambacho “ataongea nini mbele ya Mahakama”. Tumeongea mara nyingi kuhusu hili kuwa kuna sababu ipo ya kumpatia mtu nyaraka za ushahidi kupitia commital. Na wasipokuwa wamefanya (hivyo) upo mlango mwingine wa wao kuomba kupitia kifungu cha 289 cha Criminal Procedure Act.

Wakili wa Serikali: Kama namwelewa Mtobesya anazumgumzia sasa kwamba documents kutosomwa.

Jaji: Kama nimekuelewa umesema haipo kwenye Commital Bundle.

Mtobesya: Nimesema haipo kwenye Commital Bundle, na kwa maana hiyo haijakidhi matakwa hayo ya kwenye 246 CPA.

Jaji: Umeridhika na line yake ya argument sasa?

Wakili wa Serikali: Hapana! Sikubaliani na Mtobesya. Yeye ana- argue kwamba haijasomwa. Maana akianza kujielekeza kwenye mengine na mengine inakuwa siyo sawa.

Jaji: Hoja yao ni kwamba u- argue kwa namna ambayo umeletea pingamizi.

Mtobesya: Kwa sababu haipo, ina maana haijasomwa, na kwa sababu haijasomwa, inakiuka sheria aliyosoma kaka yangu Kidando ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2016. Kingine kaka yangu anasema P. O imeletwa kinyume na sheria kwa sababu ilishapitwa. Hiyo siyo sawa. Jambo lolote linaweza kuibuliwa pale tu tunapoona tunaenda kinyume cha Sheria. Tunalo hilo jukumu kama wawakilishi wa wateja wetu na pia kama maafisa wa Mahakama.

Mtobesya: Kwa hiyo kama ilivyoombwa mwanzoni Mahakama itoe maelekezo na kukidhi matakwa ya Sheria. Na pia Mahakama ielekeze uwepo wa shahidi huyu. Sisi tunasema aondoke. Ni hayo tu kwa sasa Mheshimiwa Jaji.

(Jaji anainama na kuandika kidogo. Kisha ananyanyua kichwa na kusema).

Jaji: Nimesikia hoja zote. Naomba nipate muda na mimi.

Jaji: Nitapitia Sheria zote ambazo mmezitaja. Tutarudi tena saa tano na robo.

Jaji ananyanyuka na kuondoka.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!