November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya Mbowe: Mrajisi leseni za bunduki aanza kutoa ushahidi

Spread the love

 

ASKARI Polisi, SSP Sebastian Madembwe (46), ambaye ni Mrajisi wa leseni za bunduki wa Jeshi la Polisi anatoa ushahidi wake katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ni leo Alhamis tarehe 4 Novemba 2021, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, iliyopo Mawasiliano jijini Dar es Salaam, mbele ya Jaji Joackim Tiganga anayeisikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya kigaidi.

Shahidi huyo wa sita upande wa Jamhuri, anatoa ushahidi huo akiongozwa na Wakili wa Serikali, Pius Hilla ambapo amedai yeye ni afisa wa polisi, anayefanya kazi katika Jeshi la Polisi, Makao Makuu Dodoma, Kamisheni ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, kitengo cha udhibiti na usajiliwa silaha za kiraia.

Alipoulizwa na Wakili Hilla, cheo chake katika kitengo hiko, amejibu akidai yeye ni Mrajisi wa leseni za bunduki na kwamba majukumu yake ni kupokea na kukagua maombi ya watu wanaoomba umiliki wa silaha.

Pia, jukumu lake ni kutoa vibali vya uingizaji silaha nchini, usafirishaji silaha nje ya nchi, upitishaji wa silaha kwenda katika nchi jirani kupitia nchini, kutoa vibali vya uuzaji wa silaha na risasi.

“Yote yanahusiana na usajili wa silaha. Tunahusika pia na nchi mbalimbali katika udhibiti wa silaha katika kutekeleza mikataba ya kikanda na kimataifa,” amedai Mwadembwe

Wakili wa Serikali: Umesema usajili wa kiraia. Je, unamaanisha nini?

Shahidi: Ni zile silaha zilizoruhusiwa kwa mujibu wa Sheria namba 02 ya mwaka 1995. Sheria imetaja silaha zinazoruhusiwa ni bastola, riffles, short gun na silaha yoyote ambayo Bodi ya Udhibiti wa Silaha itapendekeza iingie miongoni mwa silaha za kiraia. Samahani Mheshimiwa Jaji, silaha nyingine ni gobole.

Mbali na Mbowe kwenye kesi hiyo, wengine ambao walikuwa makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Hassan Bwire, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Mbowe na wenzake wanadaiwa kula njama za kufanya vitendo vya ugaidi, ikiwemo kulipua vituo vya mafuta na kufanya fujo katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi, pamoja na kudhuru viongozi wa Serikali, akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.

Mwanasiasa huyo na wenzake wanadaiwa kupanga njama za kutenda vitendo hivyo mwaka jana, kwa lengo la kuonesha kuwa Serikali imeshindwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Hadi sasa, mahakama hiyo imepokea vielelezo tisa vya ushahidi wa upande wa mashtaka, ikiwemo maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili, Kasekwa.

Silaha aina ya bastola, risasi tatu, maganda ya risasi, barua ya Kampuni ya Mawasiliano ya MIC Tanzania Ltd (Kampuni ya Tigo), kuhusu taarifa za miamala ya fedha ya namba inayodaiwa kuwa ni ya Freeman Aikael Mbowe na taarifa ya utambulisho wa namba hiyo.

Kielelezo kingine ni, barua ya Kamishna wa Polisi wa Upelelezi wa Kisayansi, kwenda katika Kampuni ya Mawasiliano ya Tigo, ikiomba taarifa za miamala ya fedha ya namba inayodaiwa kuwa ni ya Mbowe, kwa ajili ya uchunguzi.

Kwa upande wa mashahidi, Jamhuri umeleta mashahidi sita, kati ya 24 iliyopanga kuwaleta mahakamani hapo katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi, yenye mashtaka sita ya kula njama za kufanya vitendo vya ugaidi.

Mashahidi wengine waliotoa ushahidi wao ni, Mwanasheria wa Kampuni ya Mawasiliano ya MIC Tanzania Ltd (Kampuni ya Tigo), Fredy Kapala. Anita Varelian, Koplo Hafidhi Abdllah Mohammed, Justine Elia Kaaya na Kamanda wa Jeshi la Polisi Kinondoni, ACP Ramadhan Kingai.

Mashahidi hao walitoa madai mahakama hapo juu ya namna Mbowe alivyosuka mipango hiyo, ikiwemo kutafuta makomandoo wa JWTZ, kutuma fedha zinazodaiwa kuwa na lengo la kufadhili vitendo vya ugaidi na namna alivyokutana na washtakiwa wenzake kupanga njama za kufanya vitendo vya ugaidi.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali

error: Content is protected !!