December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya Mbowe: Mshtakiwa aeleza alivyokamatwa, kuteswa na kubadilishwa jina

Spread the love

 

MOHAMED Abdillah Ling’wenya, ambaye ni mshtakiwa wa tatu katika kesi ya ugaidi inayomkabili yeye na wenzake watatu akiwemo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameieleza Mahakama jinsi alivyokamatwa, kuteswa na kufikishwa kortini na Jeshi la Polisi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ling’wenya (35) ameelezea hayo leo Alhamisi, tarehe 25 Novemba 2021, alipokuwa akitoa ushahidi wake, katika kesi ndogo ya kupinga maelezo ya onyo yanayodaiwa kuwa yake kupokelewa mahakamani kama kielelezo cha mahakama.

Shahidi huyo wa kwanza upande wa utetezi, alikuwa akiongozwa na wakili Dickson Matata kutoa ushahidi katika Mahakama ya Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi iliyopo Mawasiliano jijini Dar es Salaam mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Mbali na Mbowe na Ling’wenya kwenye kesi hiyo, wengine ni Adam Kasekwa na Halfan Bwire ambao kwa pamoja, wanatuhumiwa kupanga njama za vitendo vya ugaidi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo kudhulu viongozi wa serikali na kulipua vituo vya mafuta na kukata miti barabara ya Morogoro- Iringa ili isipitike.

Ling’wenda ambaye alikuwa komandoo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) amedai mahakamani hapo kwamba, alikamatwa yeye na mwenzake, Adam Kasemwa tarehe 5 Agosti mwaka 2020, eneo la Rau Madukani, Moshi mkoani Kilimanjaro.

Amedai, mara baada ya kukamatwa walipelekwa kituo kikuu cha Polisi Moshi na watu zaidi ya nane ambao hawakufahamu kama ni polisi kwa sababu hawakujitambulisha.

Amewataja baadhi ya waliowakamata ni Goodluck, Francis, Mahita, Ramadhani Kingai na Jumanne.

“Mara baada ya kufikishwa pale Central, nilipelekwa moja kwa moja selo kwenye chumba ambacho kulikuwa na watu wengi,” amedai Ling’wenya

Amedai, alitolewa selo na kupelekwa katika chumba kingine na nikawakuta “wapo na kamera zao, wamenizunguka na kuanza kuhojiwa kwamba nini kilichokuleta Moshi.”

Alipoulizwa na wakili Dickoson Matata ni nani aliyekuwa anamhoji amedai ni Jumanne na wakati mwingine Mahita.

“Wakati nawajibu kuwa nimekuja kufanya VIP Protection kwa mheshimiwa Mbowe, walikuwa wanasema wanajua kuwa sisi tunajua kilichokuleta huku wala usitudanganye,” amedai

Shahidi huyo amedei, wakati hayo yakiendelea alikuwa amefungwa pingu “na Mahita akasema huyu si hataki kusema, akachukua bomba akalipitisha katikati ya miguu na mikono, akalinyanyua juu, nikabinuka, wakati huo nyayo zikawa juu. Mahita akaanza kunipiga.”

Amedai, kufuatia kipigo hicho hata kuongea akashindwa “nikasikia sauti ya askari mmoja akisema msimpige muacheni. Nikashushwa kwenye bomba, wakaniweka chini kisha wakanirudisha tena ndani.”

Shahidi huyo amedai, tarehe 6 Agosti 2020, alitolewa akiwa amefungwa kitambaa kizito na kupandishwa katika gari ikiwa ni jioni kwani jua lilikuwa limeanza kuzama.

Alipoulizwa kwamba, walipokuwa Moshi, walizunguka maeneo mbalimbali kumtafuta mtuhumiwa mwingine amekana akidai, mara baada ya kutolewa Moshi, walisafiri na kujikuta amefikishwa kituo cha Polisi Tazara jijini Dar es Salaam.

Amedai, alijua ni Tazara baada ya wale aliowakuta kituoni hapo kuwauliza hapa ni wapi na wao wakamjibu ni Tazara na kudai katika safari yao kutoka Moshi hadi Tazara na wakati akiwa Moshi baada ya kukamatwa hakuwahi kupewa chakula.

Ling’wenya amedai, kituoni hapo Tazara alikutana na askari wenzake waliowahi kufanya kazi wote Kikosi 92KJ cha makomandoo.

Ameendelea kudai kuwa mchana wa tarehe 7 Agosti 2020, alitolewa na kupandishwa juu ya kituo hicho na kukutana na askari wale wale waliomkamata Moshi na mwingine aliyemfahamu kwani wamewahi kufanya kazi pamoja.

Amedai, tarehe 9 Agosti 2020, alitolewa na kupandishwa gari na kina Goodluck na Mahita akiwa amefungwa usoni na kufikishwa kituo cha Polisi Mbweni ambacho alikuja kukijua baadaye baada ya kuuliza mmoja wa askari aliyekuwa pale.

Ameendelea kudai kwamba, akiwa kituoni hapo alipewa kikaratasi na kuambiwa kwa sasa jina lako litakuwa Jonson John na tarehe 10 Agosti 2020, alifika mkuu wa kituo hicho ambaye ni mwanamke na akamuuliza jina lake akasema anaitwa Jonson John.

Amedai, akamweleza jinsi alivyokamatwa, alipotoka, kazini kisha mkuu huyo wa kituo akamweleza amtajie jina lake halisi na kumweleza anaitwa Mohamed Abdilah Ling’wenya na wakati akiwa hapo alikuwa akipewa Biskuti na maji na mmoja wa askari na si chakula cha mahabusu.

Amedai alikaa kituoni hapo yeye na mwenzake Adam Kasekwa hadi tarehe 19 Agosti 2020, walipopelekwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu kwa habari na taarifa zaidi

error: Content is protected !!