Spread the love

 

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, umeweka pingamizi dhidi ya kupokelewa kwa barua ya upande wa utetezi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Barua hiyo, iliandikwa kwenda kwa Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, ili kumuomba baadhi ya nyaraka kwa ajili ya kuitumia katika kesi yake ndogo.

Pingamizi hilo liliwekwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, leo Alhamisi tarehe 25 Novemba 2021, baada ya mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo, Mohammed Abdillah Ling’wenya, kuiomba mahakama ipokee kama kielelezo cha ushahidi katika kesi ndogo ya kupinga maelezo ya onyo yanayodaiwa kuwa yake.

Wakili Kidando, ametaja hoja nne za kupinga barua hiyo kupokelewa kama kielelezo cha ushahidi kutoka kwa Ling’wenya, ambayo ya kwanza ilidai shahidi huyo pamoja na barua siyo vyakuaminika.

Huku ya pili ikidai shahidi huyo ameshindwa kuonesha mlolongo wa utunzwaji na utolewaji wa kielelezo hicho (Chain of Custody), wakati ya tatu ikidai barua hiyo kutokuwa na umuhimu.

Hoja ya mwisho ilidai shahidi huyo hakujenga msingi wa kuikabidhi barua hiyo mahakamani hapo kama ushahidi.

Baada ya kutoa pingamizi hilo, Wakili Kidando aliomba ahirisho la muda ili wajipange kukazia hoja zao kisheria, ambapo Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo alikubali kuahirisha.

Awali, wakati akitoa ushahidi wake Ling’wenya, alieleza namna walivyomuandikia barua Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, ili kumuomba baadhi ya nyaraja kwa ajili ya kuitumia katika kesi yake ndogo.

Nyaraka hizo ni, stationary diary ambacho ni kitabu kinachoonesha maudhurio ya askari polisi na kitabu kinachoonesha matukio yaliyotendeka katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar ea Salaam, tarehe 7 Agosti 2021.

Ling’wenya ametoa madai hayo mahakamani hapo mbele ya Jaji Joachim Tiganga, akijitetea katika kesi hiyo ndogo ya kupinga maelezo ya onyo yanayodaiwa kuwa yake, yasipokelewe katika kesi ya msingi kwa madai hakuyatoa.

Akiongozwa na Wakili Dickson Matata, Ling’wenya amedai, walimuandikia barua RPC huyo wa Ilala, ili awape hizo nyaraka kuthibitisha kama Askari Mpelelezi Ricardo Msemwa, alikuwepo katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar ea Salaam, kama alivyodai wakati anatoa ushahidi wake.

Akitoa ushahidi wake, Msemwa alidai yeye ndiye aliyempokea Ling’wenya alfajiri ya tarehe 7 Agosti 2020, katika chumba cha mashtaka cha kituo hicho, ilhali mshtakiwa huyo anakana hakuwahi kufikishwa hapo bali alipelekwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Tazara.

Katika ushahidi wake, Ling’wenya hakuwahi kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, kwani mara baada ya kukamatwa Rau Madukani, Moshi mkoani Kilimanjaro, alifikishiwa Kituo cha Polisi Tazara kisha akahamishiwa Kituo cha Polisi Mbweni vyote vya jijini Dar es Salaam.

Shahidi huyo amedau kwamba, alipokamatwa na kuwekwa kituo kikuu cha polisi Moshi kabla ya kusafirishwa, alikutana na kipugo kutoka kwa maaskari polisi aliowataja kwa majin ya Ramadhan Kingai, Mumanne na Mahita.

Ling’wenya ameanza kutoa kujitetea leo, baada ya upande wa jamhuri kufunga ushahidi wao kwa kupeleka mashahidi wanne kati ya sita waliopanga kuwatumika katika kesi hiyo ndogo ndani ya kesi ya msingi.

Mbali na Mbwe na Ling’wenya washtakiwa wengine ni Adam Kasekwa na Halfan Bwire ambao kwa pamoja wanatuhumiwa kupanga vitendo vya kigaidi kwa kulipua vituo vya mafuta katika mikoa mbalimbali pamoja na kudhulu viongozi wa serikali.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali kujua kinachoendelea

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *