December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kicheko riba mikopo, BoT wajipanga kushusha, Rais Samia akomaa

Benki Kuu ya Tanzania (BoT)

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema amebaini kuwa ukuaji wa sekta binafsi umedorora kwa sababu mikopo haiendi sana kwenye sekta hiyo licha ya hatua mbalimbali zilizochukuliwa serikali.

Hata hivyo, Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) umesema unajiandaa kupunguza riba ya mikopo ambapo hivi karibuni benki moja baada ya nyingine zitaanza kutangaza punguzo hilo ili kuvutia sekta binafsi kukopa zaidi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Mwenyekiti wa TBA, Abdulmajid Nsekela ameisema BoT imefanya maboresho ya sera yatakayoongeza chachu ya kuzishawishi benki kupunguza riba.

Akifungua mkutano wa 20 wa taasisi za fedha nchini ulioandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) leo tarehe 25 Novemba, 2021 jijini Dodoma, Rais Samia amesema amefurahishwa na kauli hiyo kwamba Benki Kuu wamelifanyia kazi suala hilo.

“Tutasikia mkitangaza jinsi mnavyoshusha riba ili sekta binafsi iweze kukopa na wote tuendelee na maendeleo ya nchi yetu.

“Lakini niombe pia wote ambao tayari na wale ambao bado tuende tukafanye kazi ili maendeleo yaje kwa haraka zaidi,” amesema.

Rais Samia amesema Juni mwaka huu wakati anafungua jengo la tawi la BoT jijini Mwanza, aligusia suala la kupunguza riba kwamba ishuke chini ya asilimia 10 ili sekta binafsi ziwezi kukopa

Aidha, amesema katika kipindi cha miaka 60 Tanzania imepata viashiria vya maendeleo kwenye maendeleo ya mtu mmojammoja.

“Kwa mfano kupunguza kiwango cha umaskini  kutoka asilimia 28.6 mwaka 2015 hadi 26.2 mwaka jana.

“Kiwango cha maendeleo ya binadamu (HDI) kimepanda kutoka 0.37 mwaka 1990 hadi 0.52 mwaka 2018. Tumeongeza uhai wa mtu kutoka miaka 50 miaka ile hadi miaka 66 sasa.

“Kwa hiyo sisi ambao tupo kwenye 60 bado tuna tamaa ya kusonga mbele pengine kwa uwezo wa Mungu tutazidi kusonga mbele kwa sababu hali ya maisha inazidi kuwa bora zaidi,” amesema Rais Samia.

Amesema licha ya Tanzania kuingia kuingia kwenye uchumi wa kati, Serikali itaendelea kuhakikisha sera zake zinakwenda kukuza zaidi uchumi wa Taifa.

Aidha, Gavana wa BoT, Profesa Florens Luoga amesema mkutano huo umekuwa jukwaa muhimu kwa wakuu wa taasisi za fedha, wasomi na watendaji kujadili maendeleo ya sekta ya benki na fedha pamoja na uchumi kwa ujumla.

Amesema katika kipindi cha miongo minne iliyopita, wamefanya mikutano 19 kujadili masuala mbalimbali ambayo yaliakisi mahitaji ya wakati husika.

“Katika mkutano wa mwaka huu tunaufanya katikati ya janga la Uviko-19 kujadili namna ya kuimarisha uchumi na nchi inavyoweza kuimarika na matumizi ya teknolojia.

Rais Samia Suluhu Hassan

“Mambo manne yatajadiliwa ikiwamo ukuaji endelevu wa uchumi wakati na baada ya janga la Uviko-19, vipaumbele na sera mbadala, kuchochea kasi ya maendeleo ya kidijitali katika kuimarisha ukuaji endelevu wa uchumi.

“Kingine ni sarafu za kidigitali, uzoefu, vihatarishi na usimamizi na kuongeza mikopo kwa sekta binafsi baada ya Uviko 19, wajibu wa Serikali, taasisi za fedha na sekta binafsi,” amesema.

Pamoja na mengine amesema Tanzania haikuepuka athari za kiuchumi zilizosababishwa na Uviko-19 licha ya kuchukua uamuzi wa kutoweka ‘lockdown’.

“Kasi ya ukuaji wa uchumi ilipungua kufikia asilimia 4.8 mwaka 2020 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 6.8 miaka mitano iliyopita.

“Sekta ya utalii iliathiriwa zaidi na Uviko-19 kwani mapato yake yalipungua zaidi ya nusu na kufikia dola za Marekani milioni 714.5 mwaka 2020. Hali hii ilitokana na kupungua kwa idadi ya watalii asilimia 60 na kufikia watalii 620,867,” amesema.

Aidha, amesema ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ulipungua hadi kufikia asilimia 4.3 mwaka 2021 ikilinganishwa na asilimia 8.1 mwaka 2019/20 kutokana na kushuka kwa mahitaji ya mikopo na kuongezeka kwa vihatarishi vya mikopo kwa wakopaji.

Wakati Waziri Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba ametoa wito wadau wa mabenki ya kibiashara kuongeza ubunifu na kupeleka  mapendekezo ya kisera wizarani  kwake kuhusu namna ya kuongeza utoaji wa mikopo kwenye sekta binafsi.

Amesema mikopo hiyo italenga maeneo makubwa ya kiuchumi kama vile  kilimo, uvivu na sekta nyingine ambazo ni kichocheo cha ukuaji wa  uchumi.

“Pia waweke ubunifu kwa ajili ya kundi kubwa la vijana wanaoshindwa kujiajiri kwa kukosa mitaji  ya kuanzisha biashara. Hili ni kundi kubwa na tunakaribisha mawazo haya ya kisera wizarani ili tuweze kupata suluhisho la changamoto ya mitaji” amesema.

error: Content is protected !!