JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam nchini Tanzania, linaichunguza Hospitali ya Aga Khani, jijini Dar es Salaam, kwa tuhuma za kutoza gharama kubwa za matibabu. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea)
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema leo Alhamis, tarehe 18 Februari 2021 kuwa, wamepokea malalamiko kutoka kwa wananchi dhidi ya hospital hiyo.
Mambosasa amesema, malalamiko hayo yanahusu “kutoza gharama kubwa za matibabu kwa wagonjwa wa matatizo kifua (Pneumonia) ambayo hupelekea matatizo ya upumuaji.”

“Aidha wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika hospitali hiyo, pindi wanapofariki dunia kumekuwa na tabia ya kuzuia miili ya marehemu na kudai kiasi kikubwa cha fedha kinyume na maelekezo ya Serikali kupitia wizara ya afya maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto,” amesema Mambosasa
Kamanda huyo amesema “menejimenti ya hospital hiyo, inatabia mbaya ya kuzuia miili ya marehemu na baada ya kuzuia, wanalazimisha sasa kutoza bili kubwa ambayo haziendani na tiba ambazo mgonjwa alikuwa hapati.”
Wamekuwa wakifanya hivyo kwa muda mrefu na kuwafanya wahusika kwenda kuuza vitu ili waje kulipa hali ambayo ni kinyume na utaratibu wa wizara ya afya.
Amesema, baada kupokea malalamiko hayo, limefungua jalada la uchunguzi lenye kumbukumbu namba DSMZ/CID/PE/34/2021 dhidi ya malalamiko hayo.
“Uchunguzi huu utakapokamilika na kubaini tuhuma hizi hatua kali za kisheria zitachukuliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama na wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto dhidi ya hospitali hiyo,” amesema
Leave a comment