May 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lowassa: Maalim Seif ameacha ombwe kubwa

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa zamani wa Tanzania, Edward Lowassa amemtaja Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar kwamba alikuwa mwanasiasa aliyekamilika kila idara. Anaripoti Hamis Mguta…(endelea)

Lowassa amemzungumzia mwanasiasa huyo ambaye alifariki dunia jana Jumatano tarehe 17 Februari 2021, saa 5:26 asubuhi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam.

Mwili wa Maalim Seif (77), aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, unazikwa leo Alhamis kijijini kwake Mtambwe, Pemba visiwani Zanzibar.

“Nimepokea kwa mstuko mkubwa sana taarifa za kifo cha Maalim Seif,” amesema Lowassa aliyekuwa mgombea urais mwaka 2015 kupitia Chadema na kuungwa mkono na vyama vya CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.

Hayati Maalim Seif akiwa na Edward Lowassa kwenye kampeni za uchaguzi mkuu 2015

“Maalim alikuwa kaka yangu katika siasa na kiumri tumefanya kazi sote CCM, Makao Makuu. Alitufundisha wengi ujasiri wa kisiasa, usikivu, uvumilivu, unyenyekevu na kutokuyumba kwa kile unachokiamini kwa faida ya nchi,” amesema Lowassa ambaye baada ya kuhamia upinzani Julai 2015, alirejea tena CCM.

Lowassa amesema “wakati wa uchaguzi mkuu wa 2015, tulishirikiana kwa karibu mno na sote tukiwa na nia ya kuona ufa wa kisiasa na kijamii uliyokuwepo nchini tunauziba.”

Wakati Lowassa akigombea urais wa Tanzania, Maalim Seif aligombea upande wa Zanzibar ambapo amesema “tulikuwa na ndoto za kuuunda serikali za umoja wa kitaifa (coalition governments). Nina faraja kubwa kuona ameondoka hilo akiwa amelitimiza miaka mitano baadaye.

“Maalim Seif alikuwa mwanasiasa barabara, mwanasiasa aliyekamilika hakika ombwe aliloliacha ni kubwa sana,” amesema.

Akihitimisha kumwelezea, Lowassa amesema “njia pekee ya sisi viongozi na Watanzania kwa pamoja kumuenzi Maalim Seif ni kuwa na mapenzi zaidi ya kudumisha amani na maisha ya watu.

“Nitakukumbuka daima kaka yangu Maalim Seif kwa upendo na nyenyekevu wako kwa wananchi,” amesema Lowassa.

error: Content is protected !!