Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Hatma ya kesi ya uraia pacha kujulikana 31 Mei mwaka huu
Habari za Siasa

Hatma ya kesi ya uraia pacha kujulikana 31 Mei mwaka huu

Dk. Stergomena Tax, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
Spread the love

 

KESI ya kikatiba iliyofunguliwa na raia wa Tanzania waishio nje ya nchi (Diaspora), kupinga Sheria inayokataza uraia wa nchi mbili, maarufu kama uraia pacha, imenguruma mahakamani jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mbele ya majaji watatu wa Mahakama Kuu, waleta maombi kupitia kwa wakili wao, wakiongozwa na Peter Kibatala, wameiomba Mahakama, kupiga marufuku sheria inayokataza uraia wa nchi mbili.

Shauri hilo la Kikatiba Na. 18/2022, linasikilizwa na majaji Mustapha Ismail, Hamidu Mwanga na Obadia Bwegoge. Limewasilishwa mahakamani na   Shaban Fundi, Patrick Nyelesa Nhigula, Restuta Kalemera, Nkole Muya, Emmanuel Emmanuel na Bashir Kassam, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Fundi, Nhigula na Emmanuel, kwa sasa wanaishi nchini Marekani, huku  Kalemera na Muya wakiishi Uingereza. Naye Kassam yuko nchini Canada.

Katika kesi hiyo, waleta maombi, wanataka Mahakama itamke bayana kuwa vifungu vya 7 (1) na (2) (C), pamo ja vifungu vya (4) (a) na (6) vya Sheria ya Uraia ya Tanzania ya mwaka 2002 na kifungu cha 23 (1) (h) na (1) na cha 27 (2) (a) cha Sheria ya Uhamiaji ya mwaka 2016, ni kinyume na Katiba.

Baada ya kusikiliza hoja kutoka pande zote mbili – Jamhuri na waleta maombi – Mahakama Kuu, imeagiza pande zote mbili, kuwasilisha hoja za mapingamizi na majibu yake, ndani ya wiki mbili zijazo na kwamba uamuzi kuhusiana na mapingamizi hayo, utatolewa tarehe 31 Mei mwaka huu.

Akitoa maelezo hayo, Jaji Mwanga alisema, Mahakama imeagiza pande zinazohusika “kuwasilisha hoja za mapingamizi na majibu ya mapingamizi hayo,  kwa njia ya maandishi.”

Alisema, “upande wa Jamhuri unatakiwa kuwasilisha hoja zake za mapingamizi tarehe 16 Mei, huku waleta maombi wakitakiwa kuzijibu tarehe 23 Mei.”

Aliongeza, “Huku Jamhuri ikipewa nafasi ya kuwasilisha hoja za mwisho tarehe 30 Mei 2023.

Waleta maombi wote wanaeleza katika viapo vyao, kwamba vifungu wanavyovilalamikia vinakiuka Katiba ya Jamhuri kwa kuwa vinaeleza kuwa raia yeyote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anayechukua uraia wa nchi nyingine, moja kwa moja anakuwa amepoteza uraia wake wa Tanzania.

Wanasema, maelezo ya vifungu hivyo yanakwenda kinyume na Katiba kwa kuwa Katiba ya Jamhuri ya Jamhuri, hainyang’anyiki mtu haki ya kuwa raia wa kuzaliwa.

Waleta maombi wametaja katika viapo vyao, miongoni mwa haki ambazo wanazipoteza kwa kuwapo kwa sheria hiyo, ni kunyimwa haki mbalimbali katika nchi yao waliyozaliwa kwa kuzingatia kwamba walipata uraia wa nchi hizo kwa sababu za kiuchumi na ustawi wa kijamii.

Wanadai kuwa wao ni Watanzania kwa damu na kwamba wanatamani kuendelea kuwa Watanzania, lakini kwa vifungu hivyo vya Sheria ya Uraia wananyimwa haki hiyo.

Wanadai kuwa wenzao wanaotoka katika nchi nyingine za Afrika Mashariki kama vile Kenya, Rwanda na Uganda, wanaoishi nje ya nchi wanaruhusiwa kuwa hati za kusafiria za Afrika Mashariki kwa kuwa nchi zao zinaruhusu uraia pacha, lakini wao hawawezi kupata hati hizo.

Mengine wanayotaja kuyakosa kutoka kwenye nchi yao ya asili, ni kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi na kwamba wanapotembelea nchini wanaishia kuishi katika nyumba za ndugu zao au hotelini.

Haki nyingine, ni kuweza kuchagua viongozi wala kushiriki kugombea nafasi ya umma katika chaguzi zinazofanyika Tanzania.

Miongoni mwa hoja za mapingamizi ya Jamhuri katika shauri hilo linalovutia mamilioni ya wananchi, ni pamoja na kutaka Mahakama ilitupe mbali shauri hilo kwa waleta maombi hawakuweka sahihi katika hati za madai.

Hoja nyingine, ni waleta maombi kukiuka Sheria ya Kupambania Haki za kikatiba, kifungu cha nne; viapo kuapwa nje ya nchi lakini vikionekana kushuhudiwa na mawakili walioko nchini.

Suala la kuwa na uraia wa zaidi ya nchi moja, maarufu kama “uraia pacha” nchini, limechukuwa likichukua sura mpya hasa baada ya mchakato wa kupatikana Katiba mpya ukwame mwaka 2014.

Katika Rasimu ya Katiba ya Jaji Joseph Sinde Warioba, umuhimu wa kuwapo uraia pacha, ulielezwa kwa ufasaha na kukatolewa mifano kadhaa ya kuunga mkono uwapo wake.

Kesi ilifunguliwa 17 Desemba mwaka jana.

Endelea kusoma MwanaHALISI kwa habari zaidi kuhusiana na shauri hili na mambo mengine ndani na nje ya nchi – Mhariri.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Sauti ya Watanzania waeleza sababu za kuiunga mkono Chadema

Spread the love  KIKUNDI kinachojipambanua katika kupigania rasilimali na uhuru wa nchi,...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Tanzania, Somalia kuibua maeneo mapya ya ushirikiano

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Somalia...

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

error: Content is protected !!