December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Mwinyi aonyesha njia ya maridhiano Zanzibar

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi

Spread the love

RAIS wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUKI), Visiwani Zanzibar, Dk. Hussein Alli Mwinyi, amewaomba wananchi visiwani humo, kuweka kando tofauti zao za kisiasa, kwa maslahi ya taifa lao. Anaripoti Brighhnes Boaz, Dar es Salaam … (endelea).

Dk. Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumanne, tarehe 8 Desemba 2020, mara baada ya kumaliza hafla ya kumuapisha, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Katika hafla hiyo iliyofanyika Ikulu, mjini Unguja, Dk. Mwinyi ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (BLM), ameeleza kuwa ili kuijenga Zanzibar, ni sharti kuwapo kwa umoja na mshikamano.

Alimshukuru Maalim Seif ambaye ni Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo na mtu ambaye alikuwa mshindani wake mkuu katika uchaguzi uliyopita, kwa kuruhusiwa na chama chake, kushika nafasi hiyo.

Uteuzi wa Makamo wa Rais, umetajwa kwenye Katiba ya Zanzibar (1984), toleo la mwaka 2010, ambapo kumeelezwa kuwa chama ambacho kitashika nafasi ya pili katika uchaguzi mkuu uliomalizika, kitapendekeza jina la mwanachama wake kwa rais, ili kuweza kushika nafasi hiyo.

Maalim Seif ameapishwa baada ya kuteuliwa na Rais Mwinyi Jumapili iliyopita ya tarehe 6 Desemba 2020, ikiwa ni muda mufupi kupita tangu chama chake cha ACT-Wazalendo, kuwaeleza wananchi, kuwa kimeridhia kushirikiana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuunda Serikali ya Zanzibar.

Rais Mwinyi amesema, “nakushukuru Maalim Seif kwa kukubali uteuzi wangu kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais. Kwani maridhiano ni jambo linaloleta nchi pamoja, kudumisha amani na kusonga mbele kwa pamoja kama taifa.”

Dk. Mwinyi amesema, yeye na Maalim Seif wamekubali na kuonyesha njia katika maridhiano hayo na kuahidi kutekeleza kila ambacho kipo kwenye uwezo wake, katika kufanikisha hayo.

Amesema, nimeanza kutekeleza wajibu wangu. Lakini “uko wajibu wa viongozi, vyama vya siasa na wananchi, na mimi nitajitahidi kuyajenga na kuyadumisha maridhiano.”

Dk. Mwinyi amesema, “maridhiano ya kweli yanajengwa na mambo matatu; dhamira kwa pande zote mbili zinazotofautiana, ni lazima kukaa pamoja na kuzungumza; kuvumiliana, kustahimiliana na kusahau yaliyopita.” Amesema, “waswahili wanasema, yaliyopita si ndwele, tugange yajayo.”

Amesema, “kama mambo yamepita, yanahitaji kusahaulika ili kuacha kutonesha vidonga. Tunapaswa utamaduni mpya wa kuaminiana.”

Dk. Mwinyi amesema, uamuzi huo alioufanya una baraka zote za viongozi wa chama chake –  Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mwenyekiti wake, Rais John Pombe Magufuli.

Ameongeza, “sasa tutaweka pembeni tofauti zetu na tutaijenga pamoja Zanzibar yetu. Maslahi ya wananchi ndiyo kila kitu, tofauti zetu zisitugawane na wananchi tunaomba ushirikiano wao. Mafanikio na malengo yetu, yatategemea vyama vyetu katika utayari, mimi na Maalim Seif tumeonyesha utayari huo, tuijenge Zanzibar mpya yenye amani.”

Baadhi ya viongozi wa ACT-Wazalendo waliohudhulia, ni pamoja na Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Zitto Zuberi Kabwe, Makamu wenyekiti Bara na Visiwani Doroth Semu Bara) na Juma Duni Haji (Visiwani); Katibu Mkuu, Ado Shaibu na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui.

Kuapishwa kwa Maalim Seif kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, kumefanyika katika kipindi ambacho vidonda vya uchaguzi kwa wafuasi, wanachama na baadhi ya viongozi wake, vikiwa bado vibichi.

error: Content is protected !!