Thursday , 30 March 2023
Home Gazeti Habari Dk. Hoseah ajitosa urais TLS
HabariTangulizi

Dk. Hoseah ajitosa urais TLS

Dk. Edward Hosea
Spread the love

 

ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Dk. Edward Hoseah, amejitosa katika kinyang’anyiro cha kuwania urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Dk. Hoseah ambaye aliondoka Takukuru mwaka 2016, amejitosa katika kinyang’anyiro hicho, akikabiliana na wagombea wengine wanne, akiwamo Flaviana Charles, ambaye ni mwanamke pekee.

Uchaguzi mkuu wa TLS, umepangwa kufanyika tarehe 15 Aprili 2021 na tayari Baraza la Uongozi la TLS, limepitisha wagombea hao, ambao wamekwisha kuanza kampeni.

Wengine waliojitosa kwenye nafasi hiyo, ambayo kwa sasa, inashikiliwa na Dk. Rugemeleza Nshalla, ni Shehzada Walli, Albert Msando na Francis Stolla, ambaye amewahi kuhudumu katika nafasi hiyo ya urais kati ya mwaka 2016 hadi 2017.

Dk. Hoseah, ambaye ni muhitimu wa Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2007, kwa sasa ni wakili wa kujitegemea, mwenye makazi yake, jijini Dar es Salaam.

Fraviana Charles mgombea Urais TLS

Aliondoka Takukuru kwa kile ambacho mamlaka yake ya uteuzi ilidai, kutoridhishwa kwa namna taasisi hiyo, inavyotekeleza wajibu wake, katika kupambana na rushwa hususani upotevu wa mapato ya serikali katika bandari ya Dar es Salaam.

Dk. Hoseah aliongoza taasisi hiyo nyeti, kwa miaka kumi mfululizo, kuanzia tarehe 26 Novemba 2006, baada ya kuteuliwa na Rais wa wakati huo, Jakaya Mrisho Kikwete na kuondolewa 15 Desemba 2016 na Rais John Pombe Magufuli, ambaye kwa sasa ni marehemu.

Rais Magufuli, aliingia madarakani tarehe 5 Novemba 2015 na kutengua uteuzi wa Dk. Hoseah, ndani ya kipindi cha takribani mwaka mmoja.

Tangu kuondoka kwa Dk. Hoseah katika taasisi hiyo, takribani miaka minne na ushehe iliyopita, Takukuru imeongozwa na wakurugenzi watatu ambao ni, Kamishina wa Polisi, Valentino Mlowola; ambaye baadaye aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa balozi nchini Cuba.

Shehzada Walli mgombea Urais TLS

Mwingine ni aliyekuwa mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI), Diwani Athuman, ambaye sasa ni mkurugenzi wa usalama wa taifa na sasa taasisi hiyo, inaongozwa na Bregedia Jenerali John Mbungo.
Uchaguzi wa TLS, unakabiliwa na ushindani mkali kutokana kuwapo kwa wagombea wenye majina, akiwamo Stolla aliyewahi kuwa rais wa chama hicho.

Hata hivyo, Stolla alitaka kutetea nafasi hiyo mwaka 2017, lakini alijikuta anashindwa vibaya na wakili mwenzake, Tundu Antipas Lissu, aliongoza TLS kwa takribani miezi mitano kati ya 12.

Lissu ambaye wakati huo, alikuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alishindwa kumalizia muhula wake wa uongozi, baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana, tarehe 7 Septemba 2017.

Shambuli dhidi ya Lissu, lilitokea mchana akiwa katika makazi yake Area D, mjini Dodoma, wakati akitoka kuhudhuria kikao cha Bunge, kilichokuwa kikiendelea.

Mara baada ya shambulio hilo, Lissu alikuwa nje ya nchi Kenya na baadaye Ubelgiji kwa matibabu hivyo, kumfanya kushindwa kuendelea na majukumu yake ya urais wa TLS.

Uchaguzi wa mwaka 2018 ulipofanyika, Fatuma Karume, mtoto wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Aman Abeid Karume alishinda nafasi hiyo na kuwaongoza mawakili kwa mwaka mmoja hadi 2019, na kijiti kuchukuliwa na Dk. Rugemeleza Nshalla ambaye anaendelea mpaka sasa.

Naye Albert Msando kama ilivyo kwa Flaviana Charles na Shehzada Walli, wanawania nafasi hii kwa mara ya kwanza, kutaka kuongoza chombo hicho muhimu kwa mawakili.

Msando, aliwahi kuwa mshauri mkuu wa sheria wa Chama cha ACT-Wazalendo hadi tarehe 21 Novemba 2017, alipojiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), mbele ya kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho, iliyofanyikia Ikulu ya Dar es Salaam.

Albert Msando mgombea Urais TLS

Kikao hicho, kiliongozwa na aliyekuwa mwenyekiti wa CCM, John Pombe Magufuli.

Desemba mwaka 2021, Dk. Magufuli alipounda kamati ya kufuatilia mali za CCM, Msando alikuwa miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo iliyoongozwa na Dk. Bashiru Ally.

Wakati huo, Dk. Bashiru, alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye baada ya kukabidhi ripoti ya ufuatiliaji huo, Dk. Magufuli alimpendekeza kuwa katibu mkuu na wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM, walimuidhinisha, tarehe 26 Februari 2018.

Kwa sasa, Dk. Bashiru ni Katibu Mkuu Kiongozi, baada ya kuteuliwa tarehe 26 Februari 2021 na kuapishwa kesho yake yaani 27 Februari 2021 na Rais Magufuli, ukiwa ni uteuzi wa mwisho kuufanya hadi mauti yalipomfika Rais Magufuli 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

ElimuHabari

Serikali yataka vijana  wajiunge na program atamizi ya biashara CBE

Spread the love  SERIKALI imewahamasisha vijana kujiunga na program atamizi inayotolewa na...

AfyaHabari

Ugonjwa wa ajabu ulioua watano Bukoka ni Marburg

Spread the loveWAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amesema ugonjwa wa ajabu uliosababisha...

AfyaHabariHabari

Ugonjwa wa ajabu wadaiwa kuua watano Kagera, Serikali yatoa tahadhari

Spread the loveJUMLA ya watu watano wanaidaiwa kufariki dunia  katika vijiji vya...

ElimuHabari

CBE yaanzisha Shahada 10 za Uzamili, CBE yajivunia wahitimu wanaoajirika

Spread the loveCHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimewataka wenye  kampuni na...

error: Content is protected !!