July 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CUF yawasilisha mapendekezo kikosi kazi cha Rais kwa shingo upande

Spread the love

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimewasilisha kwa shingo upande maoni na mapendekezo yake katika Kikosi Kazi kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya kukusanya maoni yenye lengo la kuimarisha demokrasia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Hayo yamebainishwa katika taarifa ya CUF, iliyoanisha muhtasari wa mapendekezo iliyowasilisha katika kikosi kazi hicho, leo Jumanne, tarehe 24 Mei 2022.

Taarifa ya CUF imedai kuwa, licha ya mapungufu yaliyojitokeza katika kikosi kazi hicho, kimeamua kuwasilisha maoni yake kwa sababu kinaamini Rais Samia, ameonesha nia njema ya kujenga demokrasia na siasa za kistaarabu na kuheshimiana.

“Pamoja na mapungufu haya tumeamua kuleta maoni yetu kwenye Kikosi Kazi kwa sababu tunaamini Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha nia njema ya kujenga Demokrasia na siasa za kistaarabu na kuheshimiana,”

“Ni muhimu wadau wa siasa na demokrasia nchini tukampa moyo kufanya mabadiliko muafaka ili tujenge nchi yenye demokrasia na utawala bora,” imesema taarifa ya CUF.

Miongoni mwa mapungufu yaliyotajwa na CUF, ni madai ya kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kutoteua mjumbe kutoka ndani ya chama hicho.

Pamoja na kuwasilisha mapendekezo na maoni yaliyotolew akatika mkutano wa vyama vya siasa moja kwa moja kwaRais Samia, kabla ya kuwasilishwa kwenye Baraza la Vyama vya Siasa kwa ajili ya kujadiliwa.

“Msajili hakuteua mjumbe yeyote kutoka CUF kwenye Kikosi Kazi. Hatukuwa na tatizo na hilo kwa kuwa tuliamini mapendekezo ya mkutano yatarejeshwa kwenye baraza la vyama kujadiliwa. Hilo halikufanyika. Baya zaidi tulistushwa na kuibuka kwa pendekezo jipya ambalo halikuwa zao la mkutano wa Dodoma kuwa Mchakato wa kupata katiba mpya usubiri mpaka baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025,” imesema taarifa ya CUF.

Chama hicho kimekishauri kikosi kazi cha Rais Samia, kujijengea uhalali kwenye jamii na wajumbe wake kwa kuwasilisha ajenda zinazojadiliwa na pande zote.

Hadi sasa vyama vya siasa mbalimbali vimewasilisha mapendekezo yake katika kikosi kazi hicho, ikiwemo Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Chama Cha Mapinduzi (CCM), ACT-Wazalendo na Chama cha DP. Zoezi hilo bado linaendelea.

Hata hivyo, Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania-Chadema, kimegoma kuwasilisha mapendekezo yake katika kikosi kazi hicho, badala yake kimewasilisha suala hilo kwa Rais Samia moja kwa moja, kikidai hakina imani nacho.

error: Content is protected !!