September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CUF: Msajili wa Vyama afute ACT-Wazalendo

Spread the love

KISHINDO cha Maalim Seif Shariff Hamad kuhamia Chama cha ACT-Wazalendo tayari kimeyumbisha chama chake cha awali, Chama cha Wananchi (CUF). Anaripoti Jabir Idrissa … (endelea).

Hatua ya maelfu ya waliokuwa wanachama wa CUF kuhamia ACT-Wazalendo baada ya Maalim Seif, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF kujiunga nacho, imewasukuma CUF kuja na mkakati mpya.

Sasa wanaitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kukichukulia hatua ACT-Wazalendo kwa madai ya kufanya vurugu visiwani Zanzibari.

Akizungumza na waandishi wa habari visiwani humo Alhamisi ya tarehe 21 Machi 2019, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya CUF, Mussa Haji Kombo ametaka ACT Wazalendo kifutwe.

Kombo ambaye ameingizwa kwenye bodi hiyo kutokana na marekebisho yaliyofanywa mara baada ya CUF kuunda bodi mpya amedai, ACT Wazalendo kinafanya vurugu na hujuma dhidi ya chama chao.

Kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip iliyopo nje kidogo ya mji wa Zanzibar amesema, ACT-Wazalendo imekwenda na vurugu visiwani humo.

“Hawa wamekuja na vurugu pamoja na vitendo vya kuhujumu mali za chama chetu, kwa hivyo tunataka msajili wa vyama va sisasa akifute chama hiki cha ACT-Wazalendo,” ameseam Kombo.

Kwenye mkutano huo, Abas Juma Muhinzi ambaye ni makamu mwenyekiti mpya wa CUF amemtaja Maalim Seif kuwa kiongozi mzuri na mwenye historia ya kutukuka.

“Maalim Seif ana historia ya kuwa kiongozi mzuri lakini akiwa CUF alivurugwa na wasaidizi wake wengi aliokuwa akiwaamini,” amesema.

Tuhuma dhidi ya ACT Wazalendo zinakuja sasa ambapo chama hicho kinapokea wanachama na viongozi waliokuwa wakihudumu CUF tangu kuasisiwa kwake na Maalim Seif miaka 27 iliyopita.

Wimbi hilo lilianza Jumatatu wiki hii, wakati Maalim Seif alipohamia ACT-Wazalendo baada ya kueleza kuchoshwa na mgogoro uliochongwa na serikali pia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Maalim Seif alitangaza kuondoka CUF saa chache baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam kutoa uamuzi kuwa, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini hakukosea kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti wa CUF.

Uamuzi huo uliotolewa na Jaji Benhajji Masoud ulikuja katika kesi ambayo CUF upande wa Maalim Seif waliifungua kupinga uamuzi wa Msajili Jaji Francis Mutungi kumtambua Prof. Lipumba.

Ni baada ya Prof. Lipumba kujirudisha madarakani miezi 10 baada ya kuwa nje kwa kujiuzulu kwa hiari yake tarehe 5 Agosti 2015 kwa madai ya kutopata ushirikiano kutoka kwa viongozi wenzake.

Kwa mara ya kwanza jana Maalim Seif aliwasili Zanzibar akifuatana na Zitto, Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo na walipokewa kwenye ofisi za Vuga, zilizokuwa zikitumiwa na CUF.

Akiwa kwenye ofisi hizo Zitto amesema anawakaribisha wanachama wa CUF kujiunga na ACT Wazalendo.

“Nimewaambia nawakaribisha sana ACT Wazalendo kwa sababu ni chama kinachokusudia kuleta maendeleo makubwa ya kiuchumi. Tunataka pia kuisaidia Zanzibar kujenga uchumi wake. Watanzania jiungeni nasi kwani mna uhuru wa kuamua chama mkitakacho,” amesema.

error: Content is protected !!