May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CUF, ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi na Chadema wasusia kikao cha msajili, IGP Sirro

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi

Spread the love

 

MKUTANO ulioitishwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania, huwenda unaweza usifanyike baada ya baadhi ya wahusika kutangaza kuususia. Anaripoti Victroria Mwakisimba, TUDARCo … (endelea).

Lengo la mkutano huo ni kuwakutanisha wadau wa vyama vya siasa, msajili na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kujadili namna bora ya kuendesha shughuli za kisiasa.

Ni baada ya kuwapo kwa malalamiko hususan kutoka vyama vya upinzani kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara na au ile ya ndani ambayo Katiba na sheria inawaruhusu.

Msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi ameitisha mkutano huo, tarehe 21 Oktoba 2021 jijini Dodoma.

Tayari vyama vinne vya upinzani vyenye nguvu nchini Tanzania- Chama Cha Wananchi (CUF), ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) vimetangaza kutoshiriki kikao hicho.

CUF na ACT-Wazalendo wametoa sababu ya kutoshiriki ni kwenda kuhudhuria kongamano kubwa la kitaifa kujadili amani, haki na maridhiano lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).

TCD inaundwa na vyama vitano vya CCM, NCCR-Mageuzi, ACT-Wazalendo, CUF na Chadema vyenye wabunge, wawakilishi na angalau madiwani watatu.

Kongamano hilo, limepangwa kufanyika kwa siku mbili tarehe 21 na 22 Oktoba 2021 jijini Dar es Salaam na inatarajiwa mgeni rasmi kuwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

NCCR-Mageuzi na Chadema vimetoa sababu vikisema, haviwezi kwenda kwenye kikao kujadili uvunjaji wa Katiba na sheria ambayo inawaruhusu kuedesha shughuli zao za kisiasa ikiwemo mikutano ya hadhara.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano ya Umma wa NCCR-Mageuzi, Edward Simbeye akizungumza na MwanaHALISI Online leo Jumapili, tarehe 26 Septemba 2021 amesema “sisi msimamo wetu, kikao kati ya msajili na jeshi la polisi, hakina umuhimu wowote.”

“Msajili nimtendaji na jeshi la polisi ni mtekelezaji, katika kundi hili hakuna watunga sera…yaani tunakwenda kufanya kikao na msajili na jeshi la polisi kuwa tufanye kikao au tusifanye, wakati Katiba na sheria inaruhusu, kwa hiyo hatutashiriki kikao cha aina hiyo,” amesema Simbeye

Simbeye amekumbushia kile kilichoelezwa na Rais Samia tarehe 28 Juni 2021 alipozungumza na waandishi na wahariri Ikulu ya Dar es Salaam kuhusu mikutano ya hadhara na ile ya ndani.

“Tarehe 28 Juni, Rais Samia aliulizwa kuhusu vikao vya ndani, alisema vikao vya hadhara visubiri, vikao vya ndani ni vya kikatiba hivyo hatuwezi kuzuiwa, lakini sisi NCCR-Mageuzi ni wahanga kwa kuzuiwa kikao cha kikatiba cha kamati kuu.”

Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF

“Kwa maana hiyo, jeshi la polisi ni watuhumiwa kwetu. Jukumu letu ni kuilinda katiba. Kwenda kujadili kuivunja Katiba ni uhaini,” amesema Simbeye

Kikao ambacho Simbeye anakizungumzia, kilikuwa kifanyike tarehe 28 Agosti 2021 katika ukumbi wa Msimbazi Center, jijini Dar es Salaam, lakini kilizuiwa na polisi.

Msimamo wa NCCR-Mageuzi, unafanana na ule uliotolewa na Chadema, Jumanne ya tarehe 7 Septemba 2021 kwamba hakiko tayari kukutanishwa na polisi kwani wamekuwa wanavunja sheria za nchi.

John Mrema, Mkurugenzi wa Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema aliwaeleza waandishi wa habari kwamba, zaidi ya miaka sita, polisi wamekuwa wakiwafanyia mambo kinyume cha Katiba na sheria na kwa matendo hayo wanapaswa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Kwa upande wa ACT-Wazalendo, leo Jumapili imetoa sababu tatu za kutoshiriki kikao hicho.

James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi

Taarifa ya chama hicho, imetolewa na Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, Salim Bimani ikisema, baada ya tafakuri ya kina, wamekubaliana kutoshiriki kikao hicho huku wakitoa hoja tatu.

Mosi; tarehe 21 hadi 22 Oktoba 2021, viongozi wakuu wa ACT Wazalendo watakuwa kwenye mkutano mkuu wa kitaifa wa haki, amani na maridhiano ulioitishwa na Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD).

Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na Rais Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Pili; baada ya msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi kutangaza kikao cha polisi na vyama vya siasa, ACT Wazalendo kupitia Kiongozi wa chama, Zitto Kabwe walimwandikia msajili kuwa kikao hicho kimjumuishe Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye ndiye mwenye dhamana ya kisiasa ya Jeshi la Polisi.

“Hadi sasa hatujapata mrejesho wa suala hilo na mwelekeo ni kuwa kikao hicho kitakuwa cha Polisi na vyama vya siasa pekee,” amesema Bimani.

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo

Tatu; 
 Bimani amesema “matamshi ya IGP Simon Sirro baada ya kikao chake na msajili wa vyama vya siasa hayaoneshi nia njema ya kikao hicho.”

“Kauli yake kuwa nchini Tanzania hakuna shida kuhusu mikutano ya nje na kwamba tatizo lipo kwenye mikutano ya ndani na inabidi sheria iwekwe sawa ni dalili ya wazi kuwa kikao hicho kinaweza kutumika kubinya zaidi shughuli za kisiasa nchini,” amesema.

Sababu za ACT-Wazalendo zinafafa na zilizotolewa jana Jumamosi na CUF kinachoongozwa na Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba.

CUF kimesema, kutokana na mwingiliano wa tarehe, wao walikwisha kujipanga kwenda kushiriki kongamano la TCD.

“CUF hatuna taarifa yoyote rasmi tokakwa msajili bali tumeiona taarifa hiyo kwenye vyombo vya habari wakati tukiwa katika maandalizi ya kushiriki kongamano kubwa la kujadili amani, haki na maridhiano,” imeeleza taarifa ya CUF iliyotolewa na kurugenzi ya habari, uenezi na mahusiano na umma.

error: Content is protected !!