MSEMAJI Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa amesema, idadi ya wananchi waliochanjwa chanjo ya corona imefikia 400,000. Anaripoti Victoria Mwakisimba, TUDARCo … (endelea).
Msigwa amesema hayo leo Jumapili, tarehe 26 Septemba 2021, wakati akizungumza na waandishi wa habari, mkoani Singida kutoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa mambo mbalimbali yaliyofanywa na serikali.
Chanjo hiyo ni kati ya milioni moja aina ya Johnson & Johnson, msaada kutoka nchini Marekani ambayo, ilizinduliwa tarehe 28 Julai 2021 na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Ikulu ya Dar es Salaam kwa yeye mwenyewe kuchanjwa.
Msigwa amesema, tangu zoezi za uchanjaji wa chanjo ya corona ilipoanza, wananchi 400,000 wamechanjwa kati ya chanjo milioni moja iliyowasili nchini “kwa kasi tunayokwenda nayo haziwezi kuchukua muda mrefu.”
Amesema, hawataki kuona Mtanzania aliyetayari kupata chanjo anapata shida ya kwenda sehemu ya kuchanjwana hivyo vituo vya chanjo vimeongezwa kutoka mia tano na kufikia zaidi ya elfu sita kwenye vituo vya mabasi, masoko, vituo vya kupima uzito magari na Mwenge wa uhuru.
“Juhudi za mapambano ya corona inaendelea na sasa kila kituo cha chanjo zaidi ya elfu sita nchini napo wanatoa chanjo ya corona kama vituo vya mabasi na hata jana kwenye mchezo wa watani,” amesema Msigwa
Msemaji huyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo amesema, “Serikali imeagiza chanjo nyingine ya corona milioni mbili kutoka China, hizi zitakuwa dozi mara mbili.”
Ametumia fursa hiyo, kuwaomba wananchi kujitokeza maeneo yenye chanjo na kuchanjwa kwani “sehemu kubwa wanaopumua kwa msaada wa mashine kwenye hospitali wengi ni ambao hawakuchanjwa.”
“Usipochanjwa yakikupata hoi na hata idadi ya vifo, vingi ni wale ambao hawakuchanja,” amesema Msigwa
Leave a comment