CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema mazungumzo aliyofanya Makamu Mwenyekiti wake Bara, Tundu Lissu na Rais Samia Suluhu Hassan, jijini Brussels, Ubelgiji ni ya chama hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo Ijumaa, tarehe 18 Februari 2022 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.
“Sisi ni waumini wa mazungumzo, kwa maana nyingine mazungumzo aliyoyafanya Lissu ni mazungumzo ya chama. Lakini tutazungumza na tunaozungumza nao tunawataka wakati wote, waweke unafiki pembeni wasimamie ukweli na haki katika mazungumzo,” amesema Mnyika.
Hata hivyo, Mnyika amesema, Chadema kinapofanya mazungumzo na Serikali, haiwazuii kuendelea na mapambano.
“Lakini kushiriki kwetu mazungumzo na milango yetu iko wazi, ya mazungumzo lakini hatuzuiwi kuendelea na mapambano ya njia nyingine za demokrasia.,” amesema Mnyika.
Katibu Mkuu huyo wa Chadema, amesema wanasubiri Rais Samia atimize ahadi yake aliyoitoa bungeni mwaka jana, ya kufanya mazungumzo rasmi na chama hicho.
“Tutashiriki mazungumzo wakati wote tutakapoona yanaleta matokeo. Mimi kwa imani yangu kwa upepo uliotoeka leo, Rais akirejea Tanzania, bado atatimiza ahadi yake aliyoitoa bungeni kwamba atafanya mazungumzo nasi,” amesema Mnyika na kuongeza:
“Tunasubiri kuendelea na mazungumzo awamu ya pili, mpaka kieleweke.”
Rais Samia alifanya mazungumzo na Lissu, juzi Jumatano, ambapo alipokea maombi matano kutoka kwa makamu mwenyekiti huyo wa Chadema, aliyoahidi kuyafanyia kazi.
Miongoni mwa mambo hayo, ni kesi ya ugaidi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe na wenzake, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam.
Mengine ni upatikanaji wa katiba mpya, tume huru ya uchaguzi na ondoleo la zuio la mikutano ya vyama vya siasa vya upinzani.
Leave a comment