KAMATI Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imekutana kujadili hali ya kisiasa nchini, ikiwemo mkataba wa ushirikiano kuhusu uendeshaji bandari, ulioingia baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam… (endelea).
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, wakati akizungumza na wandishi wa habari kuhusu ajenda zitakazojadiliwa katika kikao cha kamati hiyo kilichoketi leo Jumamosi, jijini Dar es Salaam.
Mbali na kujadili mkataba wa bandari, Mnyika amesema kikao hicho kitajadili mazungumzo kati ya Chadema na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Kikao cha Kamati Kuu kina ajenda mbalimbali, muda huu tunaendelea na ajenda ya taarifa ya hali ya kisiasa ikiwepo mkataba wa bandari na mazungumzo kati ya Chadema na CCM,” amesema Mnyika.
Serikali ya Tanzania, kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Serikali ya Dubai, kupitia kampuni yake ya Dubai Port World, imeingia makubaliano ya kuendesha bandari nchini, ambao umeibua mjadala mkali kwa baadhi ya watu kudai baadhi ya vifungu vyake vinakiuka maslahi ya taifa.
Miongoni mwa hoja zikizoibuliwa na wanaopinga mkataba huo, ni kutokuwa na Muda mahususi wa utekelezaji, kuwa na kifungu kinachozuia mkataba huo kuvunjwa, pamoja na kutoanisha maslahi ambayo nchi itapata.
Hata hivyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, jana Ijumaa aliwatoa hofu wananchi akisema mkataba huo ni wa awali na kwmaba kuna kipengele kinachoruhusu kuvunjika endapo kutatokea dosari yoyote.
Pia, Waziri Majaliwa alisema Serikali haijauza bandari, badala yake imetafuta mwekezaji kama ilivyofanyika katika Kampuni ya TICS na kwamba DP World kupitia mikataba ya utekelezaji miradi itakayoingiwa itapewa Muda wa utekelezaji kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake.
Waziri Majaliwa alisema DP World haitapewa bandari zote bali ni baadhi ya sehemu katika bandari.
Leave a comment