Friday , 1 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa CDA wazidi kubanwa, sasa kuchunguzwa
Habari za SiasaTangulizi

CDA wazidi kubanwa, sasa kuchunguzwa

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, William Lukuvi
Spread the love

WAKATI Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, akikiri kwamba kuna utapeli unaodaiwa kutekelezwa na baadhi ya watendaji wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), baadhi ya wananchi wameitaka serikali kuunda timu ya kuwachunguza watumishi wa mamlaka hiyo iliyovunjwa, anaandika Dany Tibason.

Waziri Lukuvi, alionyesha mapungufu hayo alipokuwa akizungumza na wajumbe wa chama cha wachoraji wa ramani mjini Dodoma hivi karibuni, huku wananchi wa Dodoma wakimuomba Waziri Mkuu, kuunda tume ya kuwachunguza watendaji waandamizi wa Iiliyokuwa CDA.

Wakizungumza na MwanaHALISI Online, baadhi ya wananchi hao wamedai kwa vile wao mara kadhaa walikuwa wakilalamikia suala hilo kwa waziri huyo, ni vyema sasa tume ikaundwa kuwachunguza watumishi hao waliosababisha uopotevu wa viwanja zaidi ya 34,000 vilivyopimwa kutokana na mashamba ya wananchi hao.

Emmanuel Kusekwa, mkazi wa Kisasa, amesema hatua ya Waziri Lukuvi, kukiri kuwapo kwa mapungufu hayo katika mamlaka hiyo iliyovunjwa, imefungua milango kwani wananchi wengi wa Dodoma walikuwa wakilalamikia kuporwa kwa maeneo yao, bila hata kulipwa fidia.

Jeremiha Kandambila, mkazi wa Nkuhungu, amesema CDA ilikuwa kichaka cha wanyang’anyi na wala sio mamlaka ya kustawisha makao makuu, hatua ambayo kwa sasa imeanza kujidhihirisha kwa baadhi ya viongozi wa serikali, akiwamo Lukuvi, ambao hapo awali walikuwa wakitetea uwepo wake.

“Tunamshauri na kumuomba Waziri Mkuu Majaliwa Kassim, kuingilia kati suala hili, kwani madhira ambayo watumishi na hasa maafisa waandamizi na wale wa kati wa CDA imewatendea wananchi, wanastahili kuchunguzwa,” amesema Kandambila.

Aliongeza kusema kwamba, kauli kwamba wabunge wametapeliwa inaonyesha ni kwa kiasi gani, Waziri Lukuvi, hakuwa na hamu ya kujali maslahi ya wananchi waliowengi, badala yake amekuwa akiangalia kada za wabunge na watumishi wengine serikalini.

Wananchi hao wamesema na kumtaka Waziri Lukuvi, kuachana kutafuna maneno, badala yake kutoa agizo la kuchunguzwa kwa watendaji hao wa iliyokuwa CDA, na ambao sasa wanataka kupangiwa kazi kwenye idara nyingine za serikali ikiwamo Manispaa ya Dodoma.

“Hawa watendaji wa iliyokuwa CDA wanaolalamikiwa na Waziri Lukuvi, kwamba wamesababisha upotevu wa viwanja 34,000 na kuwatapeli wabunge baadhi ya viwanja vyao, wamekuwa wakitwaa maeneo yetu bila hata kutulipa fidia, hatua hii ni mbaya na imetuumiza sana,” amesema Monica Mbuzalo, mkazi wa Kikuyu.

Wamesema, pamoja na kulalamikia mambo hayo kuanzia kwenye ngazi ya wilaya na mkoani, lakini kila mahali walipopita hawakuweza kupata msaada wowote badala yake wahusika walionekana dhahiri kuwatetea watendaji wa mamlaka hiyo ya CDA.

Hivi karibuni Rais John Pombe Magufuli, alichukua maamuzi magumu ya kuifuta mamlaka ya CDA iliyodumu kwa takriban miaka 44, mamlaka ambayo ilianzishwa kwa tamko la Rais mwaka 1973, huku ikielezwa kuwapo kwa migongano ya kimamlaka baina ya Manispaa na CDA na malalamiko ya wananchi kulichangia suala hilo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Rais mstaafu Mwinyi afariki dunia

Spread the loveRais Mstaafu wa awamu ya pili wa Tanzania, Ally Hassan...

Habari za Siasa

Waziri mkuu Ethiopia atua Tanzania

Spread the loveWaziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia,...

Habari za Siasa

Babu Owino: Vijana msibaki nyuma

Spread the loveMbunge wa Embakasi Mashariki nchini Kenya, Paul Ongili Owino maarafu...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia: Hatutazuia watu kuingia barabarani

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itaendelea kuruhusu vyama...

error: Content is protected !!