May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

CAG kutumia maabara kufanya ukaguzi, uchunguzi

Emanuel Philipo, Mchumi kutoka ofisi ya CAG

Spread the love

 

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) nchini Tanzania ameanza mchakato wa kutumia maabara katika kufanya kaguzi mbalimbali za maendeleo ikiwemo ya miundombinu ya ujenzi. Anaripoti Ibrahim Yamola, Dodoma … (endelea).

Lengo ni kuhakikisha wanakwenda na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ili kuhakikisha ripoti zinazoandaliwa kila mwaka zinakuwa na ubora wa kimataifa.

Hayo yamesemwa na Emanuel Philipo, Mchumi kutoka ofisi ya CAG leo Jumanne, tarehe 31 Agosti 2021jijini Dodoma, katika warsha ya wadau mbalimbali wa ofisi hiyo wakiwemo waandishi wa habari na asasi za kiraia kuhusu toleo maalum kwa wananchi na ukusanyaji maoni.

Philipo akitoa mada ya mpango mkakati wa miaka mitano 2021/22-2025/26 ulioanza kutekelezwa tarehe 1 Julai 2021, amesema wanakusudia kuboresha kaguzi ziweze kuendana na kaguzi za kimataifa kwa kufunga maabara mbili ya kiuchunguzi na kiufundi.

“Maabara ya kiuchunguzi, tayari ofisi iko kwenye manunuzi na tayari mkandarasi amekwisha kupewa mkataba na tunategemea tarehe 13 Septemba ataanza kuifunga na maabara ya ukaguzi wa kiufundi tuko kwenye manunuzi kununua vifaa. Tunategemea kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha, tutaanza kutumia maabara hizi mbili,” amesema Philipo.

Amesema, maabara hizo zitawafanya mathalani wanapokwenda kukagua barabara na kukuta iko chini ya kiwango, hawatalazimika kutindua bali watachukua sampuli na kuzipeleka maabara.

Katika miaka mitano ijayo, Philipo amesema, wanalenga kufanya kaguzi za hesabu kila mwaka chini ya Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma.

Kufanya kaguzi za ufanisi, kupanua mawanda ya ukaguzi katika eneo la uchimbaji wa madini, mafuta na gesi, kuimarisha ukaguzi wa kiuchunguzi na kiufundi pamoja na kuwajengea uwezo wabunge kuhusu uelewa na tafsiri ya ripoti za ukaguzi za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali pamoja na majukumu yake.

“CAG kapewa jukumu la kufanya ukaguzi, lakini anayezichambua ripoti hizi ni kamati za Bunge za PAC (Hesabu za Serikali) na LAAC (Hesabu za Serikali za Mitaa) na kamati zina wajumbe tofautitofauti, wengine ni wahasibu na wengine hawana taalamu ya mahesabu, kwa hiyo ili waweze kuchambua vizuri, lazima tuwajengee uwezo kila mwaka,” amesema.

Malengo mengine; ni kufanya ukaguzi maalum kulingana na mahitaji ya CAG, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) pamoja na wadau wengine.

“Kuhuisha mifumo inayotumiwa na wakaguzi (Upgrading TeamMate Software, ACL, Audit data lab). Hii ni pamoja na shughuli zote za ofisi kufanyika kwa njia ya mtandao (Transformation and Digitalization of Business processes) ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi,“ amesema.

Mchumi huyo amesema, katika kipindi hicho cha miaka mitano, wanashabaha ya kufanya kaguzi 330 chini ya wizara, 245 idara za Serikali zinazojitegemea, 170 Wakala na Taasisi za Serikali.

Pia, kaguzi 210 za Balozi na Jumuiya za Afrika Mashariki, kaguzi 130 za sekretariati za mikoa,kaguzi 375 za miradi ya maendeleo, kaguzi 925 za Halmashauri, kaguzi 960 mashirika ya umma, kaguzi 60 za ufanisi na kaguzi za kiuchunguzi.

error: Content is protected !!